Jumanne, Agosti 12, 2014

TANZANIA NA A/KUSINI NDIZO ZIMEJIAANDAA VEMA NA EBOLA

Tanzania na Afrika Kusini zimeelezwa kuwa nchi pekee zilizojipanga vizuri zaidi kuliko nchi nyingine katika eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya homa ya Ebola. Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Kebwe Stephen, amesema kuwa hiyo ni kutokana na mifumo mizuri ya huduma za afya iliyopo katika nchi hizo. Amesema kuwa, pamoja baada ya kuwapo mlipuko mkubwa wa ugonjwa huo katika nchi za Afrika Magharibi, Tanzania kupitia wizara yake imejipanga vizuri kuudhibiti ugonjwa huo. Hata hivyo ripoti zinaeleza kuwa, wakati ugonjwa huo ukiripotiwa kuingia Rwanda, nchini Tanzania hali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam inaonyesha hakuna udhibiti wa aina yoyote kama ilivyoahidiwa na Serikali. Katika upande mwingine, vifaa vya tiba vinavyotumika kutibu na kujikinga na ugonjwa wa Ebola, vilivyoagizwa kutoka Marekani kujikinga na ugonjwa huo hatari, viliwasili nchini mwishoni mwa wiki iliyopita na kuhifadhiwa katika Bohari ya Dawa (MSD). Dalili za awali za ugonjwa huo ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya misuli, kuumwa kichwa na kupatwa na vidonda vya kooni. Baada ya dalili hizo, mgonjwa hutapika, kuharisha, figo kushindwa kufanyakazi, kupatwa na vipele mwilini na kutokwa na damu sehemu zote za mwili zenye matundu na mwisho ni kifo.

0 comments:

Chapisha Maoni