Jumanne, Agosti 19, 2014

RADI YAUA WAWILI NA KUJERUHI WATATU

Watu wawili wa familia moja wakazi wa Kitongoji cha Kaburi, Kata ya Kanoni wilayani Karagwe, wamefariki dunia papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kupigwa na radi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe, amethibisha tukio hilo na kusema lilitokea juzi mchana baada ya mvua kubwa kunyesha ikiambatana na upepo mkali pamoja na radi.
Waliofariki dunia wametajwa kuwa ni Coletha Porotas (30) na Onesimo Nestori (14), huku waliojeruhiwa ni Emmanuel Jeremia (44), Tumsifu Emmanuel (10) na Jovinus Nestori (10), wote wakazi wa Kitongoji cha Kaburi, Kijiji cha Kanoni, Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kaburi, Willison Kristian, alisema mvua hiyo iliyonyesha kwa takribani saa moja, iliambatana na mawe, upepo mkali na radi.
Kristian alisema radi hiyo iliwakuta watu hao ndani nyumba tofauti katika kijiji hicho na kuwarusha nje.

0 comments:

Chapisha Maoni