Jumatano, Agosti 13, 2014

MADIWANI WATAKIWA KUBORESHA HUDUMA ZA JAMII IRINGA

Madiwani na watendaji wa halmashauri ya manispaa ya Iringa wametakiwa kuboresha huduma za jamii kwa kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi katika maeneo yao wanayosimamia.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Mhe. Amani Mwamwindi amesema hayo katika kikao cha baraza la madiwani kwenye ukumbi wa manispaa ambapo amesema kiwango cha ukusanyaji wa mapato katika kata mbalimbali za Manispaa ya Iringa hakiridhishi.
Mhe. Mwamwindi amewakumbusha madiwani kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki katika chaguzi mbalimbali ambayo ni haki yao ya kikatiba kutokana na uelewa mdogo wa suala hilo.
Aidha, katika kikao hicho madiwani wamefanya tathimini ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na uchaguzi wa naibu meya na viongozi wa kamati mbalimbali.
Katika uchaguzi huo Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa Bi. Theresia Mahongo amemtangaza Mhe. Gervas Ndaki kuwa naibu meya kwa kipindi kingine cha mwaka 2014/2015.
Hata hivyo, wajumbe wa kikao hicho wameshauri suala la ukusanyaji mapato kutiliwa mkazo kwa ajili ya kuendeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo ili kupunguza michango isiyo ya lazima kwa wananchi.

0 comments:

Chapisha Maoni