SERIKALI kwa kushirikiana na Taasisi ya Afrika ya Masuala ya Hisabati
na Sayansi (AIMS) kutoka Canada, wanatarajia kufungua Chuo cha Masomo
ya Hisabati ifikapo Septemba hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa kutiliana saini
mkataba na taasisi hiyo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Elimu, Profesa Sifuni Mchome, alisema lengo la kuanzisha chuo hicho ni
kulinyanyua somo la hisabati linalowashinda wanafunzi wengi.
Profesa Mchome alisema kwa kushirikiana na taasisi ya AIMS,
watahakikisha wanakamilisha ujenzi wa chuo hicho unaoendelea Bagamoyo,
Pwani, lakini kwa kuanza na wanafunzi 40 watakaosomea katika jengo la
Chuo cha Nelson Mandela kilichopo mjini Arusha.
Alisema wanafunzi hao 40 watatoka hapa nchini na nchi za jirani, ili
kuwapa uwezo na hata kujifunza mambo mbalimbali kwa lengo la
kubadilishana uzoefu kwa wanafunzi wa hapa na wa nje ya nchi.
Mkurugenzi wa taasisi ya AIMS, Thierry Zomahoun, alisema wamefanya
hivyo katika nchi mbalimbali Afrika, na kwamba maendeleo yanapatikana
kutokana na programu hizo.
Alisema masomo ya hisabati ni ya muhimu kwa kuwa hakuna taaluma isiyohusu hisabati.
0 comments:
Chapisha Maoni