Jumatano, Julai 02, 2014

WANNE WANASHIKILIWA NA POLISI IRINGA BAADA YA KUMCHOMA MOTO MWANAFUNZI WA RUCO

Watu wanne wanashikiliwa na jeshi la polisi Mkoani Iringa kwa tuhuma ya kujichukulia sheria mkononi ya kumchoma moto mwanafunzi wa Chuo cha Ruaha hali iliyopelekea kifo chake wakati akiendelea na matibabu katika hospitari ya rufaa ya Iringa.
Kamanda wa jeshi la polisi Mkoani Iringa ACP Ramadhani Mungi amesema Mussa Nganga umri wa miaka 28,Costa Mgayuka umri wa miaka 38 ,Steven Kalole umri wa miaka 24 na Samsoni umri wa miaka 24 wote wakazi wa eneo la Kihesa Manispaa ya Iringa wanashikiliwa kwa tuhuma za kifo cha Daniel Lema umri miaka 25 mwanafunzi Chuo cha Ruaha.
Kamanda Mungi ameongeza kuwa June 24 mwaka huu majira ya saa tisa usiku jeshi la polisi walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa kuna mtu anaungua moto huku mikono yake ikiwa imefungwa kwa kamba kwa nyuma ambapo aliokolewa kisha kupelekwa hospitari hali yake ikiwa mbaya.
Ameongeza kuwa tukio hilo lilitokea wakati marehemu akiwa ametoka kuangalia michuano ya kombe la dunia ila kabla ya kurejea nyumbani aliiingia Grocery iitwayo Grory eneo la Kihesa Manispaa ya Iringa ili apate kinywaji ambayo kwa mda huo ilikuwa imeshafungwa ndipo Mlinzi Musa Nganga aliwaita walinzi wenzake watatu walimkamata wakimtuhumu kuwa ni mwizi kisha wakamfanyia unyama huo.

Kamanda Mungi amesema watuhumiwa hao wamekamatwa baada ya msako mkali wa jeshi la polisi Mkoani Iringa ambapo walikimbia baada ya kutokea kwa tukio hilo aidha ametoa wito kwa jamii kutojichukulia sheria mkononi pia washirikiane na jeshi la polisi kwa ajili ya kutokomeza vitendo vya uhalifu.
Hata hivyo marehemu amefariki June 30 baada ya kuagwa na wakufunzi pamoja na wanafunzi wa chuo hicho July 01 mwaka huu mwili wake umesafirishwa Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya shughuli za mazishi ambapo alikuwa ni mwanafunzi wa mchepuo wa sheria mwaka wanne.

0 comments:

Chapisha Maoni