Jumatatu, Julai 28, 2014

KAULI YA MBUNGE CYRIL CHAMI BAADA YA MKEWE KUTUHUMIWA KUUA HOUSE GIRL

Mimi Dr Cyril August Chami, Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM) napenda kueleza masikitiko yangu kwa taarifa za uzushi na za kutunga kuwa eti mke wangu asiye na jina amemuua mfanyakazi wetu Mwislamu kwa sababu "marehemu" alikataa kwenda kanisani.
Mimi sina mfanyakazi wa jina hilo la Mariamu. Wala sina mfanyakazi mwenye umri wa miaka 16. Hatuna tatizo lolote la mfanyakazi yeyote kupigwa, achilia mbali kuuawa.
Lakini taarifa hizo ambazo ni za uongo mtupu zimewashtua wengi kwa sababu zimejengwa katika misingi ya chuki za kidini. Mtu aliyeanza kusambaza habari hiyo alilenga kuifanya jamii iamini kwamba mke wangu ambaye ni Mkristo anawalazimisha wafanyakazi wetu wasio Wakristu waikane dini yao na kuwa Wakristo. Alilenga kuibua chuki dhidi ya Waislamu na familia yangu.
Kwa hakika, mikakati hii ya kuichafua familia yangu inasababishwa na harakati za ubunge Moshi Vijijini 2015.
Wapinzani wangu wanajua wazi kuwa hawana hoja ya msingi ya kuwafanya wapiga kura wasinirudishe kwenye nafasi ya ubunge.
Kwenye jukwaa na hata kwenye medani ya maendeleo wanakwama. Kwa mfano, kabla ya barabara za lami kuanza kujengwa walisema mimi sina ushawishi wa kuifanya Serikali kuzijenga.
Sasa zimejengwa na zinaendelea kujengwa wanajenga hoja kuwa sihusiki wala Serikali ya CCM haihusiki, bali ni Benki ya Dunia inajenga!!! Wananchi wanawauliza kwani kabla ya Dr Chami kuwa mbunge Benki ya Dunia haikuwepo? Wanakosa hoja! Hivyo hivyo kwa mashule, maji, vyuo vya ufundi nk.
Kwa hiyo kwa upeo wao wanaona silaha pekee waliyo nayo ni kuzua kashfa dhidi yangu. Miezi michache iliyopita walizua nimeuza shamba la KNCU kwa shilingi bilioni 4 wakati mimi sina wadhifa wowote KNCU. Eti nimeuza nyumba mbili za Coffee Curing Moshi wakati mimi sina wadhifa wowote Coffee Curing.
Walipoona tuhuma hizo za kutunga hazijakubalika masikioni mwa wapiga kura wa Moshi Vijijini, sasa wamezua hili la mke wangu kuua ili Waislamu wa Moshi Vijijini wanione mtu nisiyefaa.

Sasa mimi napenda kuwauliza maswali haya:

Huyo mke wangu muuaji anaitwa nani? Inaingia akilini kweli kwamba mke huyo muuaji hafahamiki jina kwa hao "majirani" wetu wa kufikirika?
Binti Mariamu kauawa mji upi? Kwa nini majirani hao wenye uchungu hawajatoa taarifa kwa RPC wa mkoa au kanda husika?
Maiti kahifadhiwa hospitali ipi? Au "mke" wangu amekaa naye ndani baada ya kumuua na majirani wamekaa kimya tu?
Kwa desturi za dini ya Kiislamu binti huyo angeshazikwa sasa maana kwa mujibu wa habari hiyo ya kizushi, "aliuawa" usiku wa kuamkia jana. Je, kazikwa makaburi yapi na yako mji gani? Nani kahudhuria hayo mazishi? Kwa nini vyombo vya habari visituonyeshe hayo mazishi?
Kwa nini RPC mhusika asimkamate huyo mke wa mbunge fedhuli namna hiyo na muuaji asiyevumilika?
Kwa nini polisi hawajaniita mimi Dr Chami kunihoji kuhusu huyo "mke" wangu? Si wanajua niko jimboni Moshi Vijijini na RPC Boaz wa Kilimanjaro anafahamu niko jimboni, tena jana nimeutembelea msikiti mmoja kwa minajili ya kuutafutia umeme na maji?
Sote tunafahamu kuwa kuna mkuu mmoja wa mkoa alimuua mtu kwa kumpiga risasi na alikamatwa akapelekwa mahabusu. Huyo mke wa Dr Chami ni maarufu kuliko Mkuu wa Mkoa? Kwa nini asikamatwe tuione sura yake magazetini?
Majibu ya maswali haya HAYAPO kwa sababu kila kitu kimetungwa kwa kujenga chuki tu. Hakuna Mariamu, hakuna kipigo, hakuna kifo. Ila kuna UBUNGE WA MOSHI VIJIJINI. Ndio unaopiganiwa, hamna kingine.
Napenda kuwaasa wanasiasa wenzangu kuwa Watanzania wa leo si wa jana. Si jambo rahisi kuwaghilibu kwa staili hii. Waende kwa wananchi wachape kazi.
Wasipofanya hayo wakadhani uongo wa mitandao utawapa ubunge watashangazwa mwaka kesho 2015.
Mimi naendelea kuwaahidi wapiga kura wangu utumishi wa dhati. Nawapa pole ndugu zangu wa Kiislamu kwa usumbufu walioupata.
Waislamu wa Moshi Vijijini wananifahamu kama kiongozi nisiyewabagua kwa sababu ya dini yao. Wanafahamu kuwa nawapenda na nafahamu kuwa wananipenda sana.
Ndiyo maana wengi wamejiuliza iweje tena mke wangu amwage damu ya Mwislamu kwa sababu iliyotajwa. Naendelea kuwaahidi Waislamu wote upendo na ushirikiano siku zangu zote za kuwatumikia.
Juzi kulizuka taarifa mtandaoni kuhusu mke wa mbunge kuua mfanyakazi wake wa ndani kisa kagoma kwenda kanisani na leo mbunge katoa ufafanuzi kuhusu sakata hilo

0 comments:

Chapisha Maoni