Habari zinasema kuwa kundi la Boko Haram la nchini Nigeria
limeishambulia nyumba ya Naibu Waziri Mkuu wa Cameroon karibu na mpaka
wa nchi hiyo na Nigeria na kumteka nyara mke wake. Issa Tichiroma
Bakary, Waziri wa habari wa Cameroon na msemaji wa serikali ya nchi hiyo
amesema kuwa, kundi la Boko Haram leo limeishambulia nyumba ya Amadou
Ali, Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo katika mji mdogo wa Kolofata
kaskazini mwa Cameroon na kuuwa watu wasiopungua watatu na kumteka nyara
mke wake. Waziri wa Habari wa Cameroon ameongeza kuwa wanamgambo wa
Boko Haram pia wameishambulia nyumba ya kiongozi wa kidini katika eneo
hilo aliyetambuliwa kwa jina la Seini Boukar Lamine na kumteka nyara.
Itakumbukwa kuwa, mahakama moja ya kijeshi ya Cameroon jana iliwahukumu
kifungo cha jela kuanzia miaka 10 hadi 20 wanachama 14 wa Boko Haram.
Inaonekana kuwa shambulio hilo la leo limefanywa kulipiza kisasi cha
hatua hiyo ya mahakama ya kijeshi ya Cameroon.
0 comments:
Chapisha Maoni