IKIWA ni miezi kadhaa tangu kufanyike Bunge la Katiba kwa lengo la
kutaka kutengeneza katiba mpya bila mafanikio, taswira ya Bunge hilo
sasa imewekwa katika filamu inayotarajiwa kuachiwa mwezi ujao.
Msanii Mohamed Jongo ‘Muddy Jongo’ ndiye aliyeandika muswada na
kurekodi filamu hiyo kuonyesha mwelekeo wa mawazo yaliyokuwa
yakijadiliwa katika Bunge hilo lililofanyika mjini Dodoma.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Jongo ambaye ni dansa wa zamani
aliyekuwa akicheza muziki huku akichezea moto hadi kuwahi kuunguzwa,
alisema filamu hiyo inaonyesha unyonge wa wananchi, wabunge
waliochaguliwa kuwawakilisha wanavyowadharau na kutaka kuweka kile
wanachokitaka wao.
Alisema filamu hiyo ambayo itatoka mwezi ujao, inaonyesha jinsi
michango ya mawazo ya wananchi isivyothaminiwa, hivyo Mzee Muungaro na
wenzake kutoka Kijiji cha Amka wanajikusanya na kwenda Dodoma
kunakofanyika vikao vya Bunge kueleza msimamo wao.
Jongo aliyeandika na kurekodi filamu zenye mwelekeo wa maisha ya
kawaida ya jamii ya Kiafrika ambazo zinafanya vizuri nje ya nchi
zikiwemo ‘Fungato’ (Ficho la Uchawi) na ‘Vibration Fish’, anasema
katika filamu hiyo wameshiriki wasanii wenye majina na chipukizi ambao
wana uwezo katika tasnia hiyo.
Aliwataja baadhi ya washiriki ni yeye (Jongo), Mzee Kibinda,
Mikurupuko, Bibi Waiti, Mama Chambele, Mbega na Kindamba. Pia yumo
mmoja wa wajumbe wa Bunge halisi la Katiba, Mama Jura.
0 comments:
Chapisha Maoni