Vigogo 12 wanaodaiwa kusafirisha dawa za kulevya wanahojiwa
katika vituo mbalimbali baada ya kutajwa kwenye orodha zilizowasilishwa
serikalini na watu mbalimbali.
Ofisa wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya
Tanzania, Januari Ntisi alisema hayo wakati akijibu maswali ya waandishi
wa habari walioituhumu tume hiyo kuwa ilishapelekewa majina ya vigogo
wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, lakini imeyakalia.
Ntisi alikuwa anashiriki kwenye mkutano wa mkuu
wa Mkoa wa Mbeya, Abbasi Kandoro na waandishi wa habari alipozungumzia
maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Dawa za Kulevya mwaka huu ambayo
hufanyika kila ifikapo Juni 26 ya kila mwaka. Kitaifa maadhimisho hayo
yanafanyika mkoani hapa na mgeni rasmi atakuwa makamu wa rais, Dk
Mohamed Gharib Bilal.
Ni kweli Serikali ilipata majina mengi ya vigogo wa dawa za kulevya, lakini katika uchunguzi yakinifu tumeanza kuwashughulikia 12 ambao wanatafutwa pia na nchi za Marekani na Ujerumanialisema.
Ntisi alisema katika kufuatilia taarifa hizo, Serikali pia ilifanikiwa kukamata tani 2.3 za dawa aina ya heroine
kwenye Bahari ya Hindi pekee kati ya Januari na Juni, mwaka huu. Hata
hivyo alisita kuwataja wanaoshikiliwa akisema mapambano yanazidi kupamba
moto kwa kuwafuatilia vigogo wengine.
Awali, mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Kandoro akizungumzia
suala la maadhimisho ya siku hiyo, aliwataka wakazi wote mkoani Mbeya
na mikoa jirani, kujitokeza kwa wingi kushiriki ili wapate elimu
kuhusu madhara yatokanayo na dawa za kulevya ili waepukane nazo. Alisema
tayari baadhi ya taasisi zimeshaanza kutoa elimu katika mabanda
yaliyopo viwanja vya maonyesho.
0 comments:
Chapisha Maoni