Jumatano, Juni 11, 2014

STORI KAMILI KUHUSU VURUGU ZA MWANZA LEO

Shughuli zote za kibiashara na kijamii zimelazimika kusimama katika jiji la Mwanza kwa zaidi ya saa 6 baada ya kutokea vurugu kubwa kati ya wamachinga na jeshi la polisi ambao wamelazimika kutumia mabomu wakati wa kuwaondoa wafanyabishara hao katika eneo la Makoroboi ambalo limezuiwa na jiji hilo kutumika kwa shughuli za biashara.
Vurugu hizo kubwa zimeanza majira ya asubuhi ambapo askari polisi wakishirikiana na askari wa jiji la Mwanza waliwataka wafanyabiashara hao maarufu kama Wamachinga kuondoka katika eneo hilo na kwenda katika maeneo waliyopangiwa na baada ya kukaidi agizo hilo ndipo polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya hatua ambayo imefanya shughuli zote katika jiji hilo kusimama kwa zaidi ya saa sita.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa mwanza mrakibu mwandamizi wa jeshi la polisi SSP Christopher Fuime, amewambia waandishi wa habari kuwa tayari jeshi la polisi limewakamata watu zaidi ya kumi kuhusiana na tukio hilo huku akisema oparesheni hiyo kuondoa wamachinga katikati ya jiji la Mwanza itakuwa ya kudumu kuanzia sasa.
Nao baadhi ya wananchi wakiwemo wafanyabiashara ambao wamekumbwa na adha hiyo wakizungumza huku wengine wakiwa wamejificha vichochoroni kwa kukimbia mabomu hayo,wamesikitishwa na hatua hiyo ya jeshi la polisi kutumia nguvu kubwa na hivyo kusababisha huduma zote za kijamii kukosekana katikati ya jiji hilo la Mwanza.

0 comments:

Chapisha Maoni