Rais Jakaya Kikwete amezitaka idara na taasisi mbalimbali za serikali
pamoja na wadau wa maendeleo nchini kutumia ipasavyo takwimu
zilizotolewa na ofisi ya taifa ya takwimu kuleta maendeleo huku
akiwataka wataalam wa mipango miji kujipanga kwa kutumia taarifa hizo
ili kuondokana na ujenzi holela.
Rais Kikwete ametoa rai hiyo jijini Dar es Saalam,
alipokuwa akizindua chapisho la tatu la taarifa za msingi za
kidemografia, kijamii na kiuchumi linalotokana na sensa ya watu na
makazi ya mwaka 2012 pamoja na matumizi ya tovuti katika kupata taarifa
mbalimbali za sensa ambapo amesema suala la chanjo limechangia kwa kiasi
kikubwa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano huku akielezea
mipango ya serikali katika kupunguza vifo vya kina mama wajawazito.
Awali akimkaribisha rais waziri mkuu Mh Mizengo
Pinda ametoa rai kwa viongozi wote wakiwemo wanasiasa kuendelea
kuhamasisha matumizi ya takwimu za sensa kwa lengo la kuboresha maisha
ya wananchi na kuongeza kuwa changamoto zipo katika kutekeleza majukumu
yaliyoainishwa katika taarifa hiyo lakini serikali inazifanyia kazi.
Kwa upande wake kamishna wa sensa ya watu na makazi
ya mwaka 2012 hajati Amina Mrisho Saidi amesema sensa ya mwaka 2012
imekuwa tofauti na miaka mingine kwani tafiti zimeweza kuibua mambo
mbalimbali ikiwemo mikanganyiko na migogoro mingi ya kiutawala na kwamba
matokeo hayo ya sensa yakitumika vizuri itaweza kutatuliwa bila kuleta
athari.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya rais mkurugenzi mkuu
ofisi ya taifa ya takwimu Bi Albina Chuwa amesema matokeo hayo yamebaini
mambo mengi katika jamii ikiwemo asilimia 33 ya kaya zote nchini
zinaongozwa na wanawake na tafiti zinaonyesha kuwa ukubwa wa kaya una
uhusiano wa moja kwa moja na umaskini huku asilimia nane ya kaya zikiwa
hazina vyoo.
0 comments:
Chapisha Maoni