Jumamosi, Juni 07, 2014

FAHAMU UMUHIMU NA FAIDA ZA KULA MBOGA MBICHI

Katika maisha ya binadamu karibu kila jambo zuri linatakiwa kufanywa kwa tahadhari au kuchunga miko yake. Bila ya kufanya hivyo, faida ya jambo hilo haitapatikana na badala yake maafa yatachukua nafasi.
Ulaji wa mboga mboga zikiwa katika hali ya ubichi au zikiwa hazijapikwa una faida kubwa kiafya. Hata hivyo, ulaji huo bila ya kuchukua tahadhari utasababisha magonjwa yanayoenea kutokana na kula vyakula vichafu.

Moto unaharibu

Ni ukweli wa miaka mingi kuwa kupika au kutumia moto katika kuandaa vyakula kuna haribu virutubisho vinavyopatikana katika mboga mboga.
Mboga za majani ambazo hazijakomaa na mbichi ni chanzo kikubwa cha vitamini na madini ya aina mbalimbali. Mboga hizo endapo zitakamuliwa na kutumiwa kama juisi, faida yake kiafya itakuwa kubwa hasa kwa wagonjwa.
Mboga mboga zinaondoa tindikali inayozalishwa wakati vyakula vingine vikisagwa tumboni kama vile nyama na jibini.
Mboga za majani za kijani ni chanzo kikubwa cha carotene ambayo inabadilishwa mwilini na kuwa vitamini A.
Mboga mboga pia, ni chanzo kizuri cha vitamini C.
Vitamini A ina kazi kubwa ya kuimarisha macho ili yaone vizuri hasa wakati wa giza.
Inasaidia pia ukuwaji na ufanyaji kazi wa chembehai na kuimarisha kinga ya mwili.
Vitamini C ina kazi nyingi ikiwemo kuimarisha ufanyaji kazi wa chembehai, inaimarisha kinga, kuponya mafua na vidonda.
Baadhi ya mboga mboga zina protini na wanga. Kwa mfano, maharage na kunde ni chanzo kikubwa cha madini ya chuma na protini. Viazi mviringo na viazi vitamu ni chanzo kikuwa cha wanga.

Wito

Siku hizi kuna kuongezeka kwa tabia ya watu kutumia mboga zikiwa mbichi kutokana na wengi kutambua umuhimu wake.
Tunawahimiza watu watumie mboga mbichi kama vile saladi na kachumbari. Wanaweza kuzitumia zikiwa zimekatwakatwa au kusagwa ili kupata juisi, lakini ni lazima kuzingatia usafi.

Tahadhari
Kwa ushahidi wa kutosha wa kisayansi, ulaji wa vyakula vibichi ambavyo havikuoshwa vizuri ni chanzo kikubwa cha magonjwa ya kuambukiza kama vile homa ya matumbo, kipindupindu, tumbo la kuhara, kuhara damu, kupata minyoo na amweba.
Kwa sababu hiyo, watu wanashauriwa kuosha vizuri mboga mboga kwa kutumia maji safi na salama. Pia, watu wale saladi na wanywe juisi ya mboga mbichi ili kupata virutubisho vingi.
Mboga mboga kama matango, nyanya na karoti, zitumike kutengeneza juisi bila ya kuondoa maganda yake. Kwa sababu maganda yana madini na protini kwa wingi.

Tahadhari nyingine

Watu wawe makini kujua mahali zilipozalishwa mboga mboga wanazizonunua. Miaka michache iliyopita, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiliwahi kufanya tafiti mbalimbali kuhusu ubora wa mboga mboga zinazozalishwa kando kando ya barabara zinazopita gari na zile zinazozalishwa katika bonde la mto Msimbazi, Jijini Dar es Salaam.
Tafiti hizo zilibaini kuwa baadhi ya mboga zilikuwa hazifai kuliwa na binadamu wala wanyama kutokana na kuwa na kemikali zinazodhuru afya.

0 comments:

Chapisha Maoni