Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha juu ya
uwezekano wa kuenea ugonjwa wa Ebola barani Afrika. Msemaji wa WHO
ameeleza kuwa, mlipuko wa ugonjwa wa Ebola magharibi mwa Afrika ambao
kwa mara ya kwanza ulishuhudiwa katika mipaka ya nchi 3 za eneo hilo,
unaripotiwa kuwa uliyakumba maeneo mengi zaidi kijiografia toka ugonjwa
huo ugunduliwe. Ameongeza kuwa, mlipuko huo haujaisha na kwamba kila
siku kesi mpya zinaripotiwa nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia, kwa
ajili hiyo nchi nyingine zinatakiwa kuchukua tahadhari.
Wakati huo huo Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mpaka
imetangaza kuwa, mlipuko wa Ebola katika nchi za Guinea, Sierra Leone na
Liberia haudhibitiki na kwamba kuna hatari ya kuenea katika maeneo
mengine.
WHO imetangaza kuwa, ugonjwa huo umesababisha vifo vya watu
566 katika nchi hizo 3 tangu ulipoanza huko Conakry mji mkuu wa Guinea.
Dalili za homa ya Ebola ni kuhara na kutapika sambamba na homa kali
ambayo pia huandamana na uvujaji mkubwa wa damu. Homa ya Ebola
huambukizwa kwa kugusa damu, jasho na kinyesi cha mtu mwenye ugonjwa
huo.
0 comments:
Chapisha Maoni