Jumamosi, Juni 14, 2014

BOSS WA TANESCO AMKANA MKEWE MAHAKAMANI

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Mhandisi William Mhando, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kuwa mshitakiwa wa pili (Eva Mhando) katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka, si mke wake.
Mhandisi Mhando alitoa madai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi, alipokuwa akisomewa maelezo ya awali katika kesi hiyo na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai.

Mhando alikiri maelezo kuwa alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco tangu Juni 2010 hadi 2012, lakini alikana maelezo kuwa mshitakiwa wa pili (Eva Stephen Mhando) ni mkewe ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Santa Clara Supply Limited.
Kwa upande wake,  Eva alikubali kwamba aliwahi kuajiriwa na Tanesco kuanzia mwaka 1982 hadi 2009, mshitakiwa wa tatu, France Mchalenge pia alikubali kwamba alikuwa mwajiriwa wa shirika hilo, wakati uchunguzi unafanyika alikuwa mhasibu mkuu na alikuwa mjumbe wa Kamati ya Tathimini ya Zabuni namba Pa/001/11/HQ/G/011 ya vifaa vya ofisi, ikiwemo printa na kompyuta.
Swai alidai mshitakiwa wa nne, Sophia Misidai aliajiriwa na Tanesco na wakati uchunguzi unafanyika alikuwa mhasibu mkuu na mjumbe wa kamati iliyofanya tathimini ya zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi katika shirika hilo. Mshitakiwa alikubaliana na maelezo hayo.
Mshitakiwa wa tano, alikubali kwamba alikuwa mwajiriwa wa Tanesco na kuwa wakati wa uchunguzi alikuwa ofisa usambazaji na alikuwa mjumbe wa kamati iliyotathimini zabuni hiyo.
Mheshimiwa Hakimu, Kampuni ya Santa Clara Supply Ltd inamilikiwa na Eva Stephen William, Fred William na Veronica Stephen Mhando, ilipata zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi yenye thamani ya sh milioni 884.5.
Mhando akiwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo na Eva akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Santa Clara Supply Ltd alisaini barua ya kuipa zabuni huku akijua wazi kwamba kampuni hiyo inamilikiwa na familia yake, pia hakujitoa kuonyesha kwamba ana maslahi na kampuni hiyo
alidai.
Wakili Swai aliendelea kueleza kuwa Mhando aliwapa zabuni hiyo mshitakwa wa pili, Eva na watoto wake kinyume na utaratibu, walitaka kuiuza kampuni hiyo kwa mtu mwingine wakati tayari walishapata zabuni ya kusambaza vifaa hivyo vya ofisi, mshitakiwa wa kwanza (Mhando) alitumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kuonyesha kwamba ana maslahi binafsi na Kampuni ya Santa Clara,” alidai Swai.
Swai alidai kwamba Eva alighushi taarifa za ukaguzi wa hesabu za Kampuni ya Santa Clara ya mwaka 2007/2008 akionyesha kuwa Kampuni ya Finx Capital House ilifanya ukaguzi.
Pia mshitakiwa huyo alighushi taarifa ya kuhamisha hisa akionyesha hisa 200 zenye thamani ya sh 10,000 zilihamishiwa kwa Eveta Shing’oma.
Eva alidaiwa kutoa taarifa ya ukaguzi wa fedha kwa Katibu wa Bodi ya Zabuni wa Tanesco akionyesha zilifanyiwa ukaguzi Desemba, mwaka 2010, akajipatia sh milioni 37.7 kutoka kwa shirika hilo.
Swai alidai Mchalange, Misidai na Naftali Kisinga walitoa taarifa katika Bodi ya Zabuni kuonyesha kwamba Kampuni ya Santa Clara walikuwa wana sifa ya kupata zabuni hiyo, walipata mkataba wa kusambaza vifaa vya ofisini wenye thamani ya sh 884,550,000. Washitakiwa hao walikana maeneo yote hayo.
Wakili Swai alieleza upande wa jamhuri unatarajia kuleta mashahidi 14 na wanawasilisha mahakamani vielelezo 18.
Hakimu Mushi aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 29-30, mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

0 comments:

Chapisha Maoni