Shirika la Afya Duniani (WHO), limejiunga katika mapambano dhidi
ya ugonjwa wa homa ya dengue kwa kuagiza vipimo 1,000 kwa ajili ya
upimaji nchi nzima.
WHO imechukua hatua hiyo kusaidia juhudi
zinazoendelea za kupambana na homa hiyo na imeagiza utafiti zaidi
ufanyike ili kutambua aina halisi ya virusi vya dengue vilivyopo nchini
kwa kulinganisha na vile vinavyopatikana katika maeneo mengine duniani.
Akizungumza jana, Ofisa wa Taaluma
na Udhibiti wa Magonjwa wa WHO, Dk Grace Saguti alisema tayari chombo
hicho kimeagiza vipimo hivyo vitakavyogharimu Sh17.7 milioni na kila
kimoja kinaweza kupima sampuli 25, hivyo kunufaisha watu 25,000.
Hatua hiyo imechukuliwa huku kukiwa na taarifa
kwamba baadhi ya hospitali za Serikali za wilaya na rufaa zinakabiliwa
na uhaba wa vipimo, hali iliyosababisha kutoza kati ya Sh25,000 hadi
Sh30,000 kwa ajili ya kupima mgonjwa mmoja.
Katika vituo binafsi, wagonjwa wamekuwa wakipimwa kwa gharama inayofikia Sh50,000 hadi 60,000 kwa kila mtu.
Juhudi hizo za WHO zimetangazwa siku moja baada ya
Serikali kupitia Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Steven
Kebwe kulieleza Bunge kuwa kwa sasa vipo vipimo 350 na Serikali
inatarajia kuagiza vingine 750.
Dk Saguti alisema WHO imeshatengeneza miongozo,
mikakati na mafunzo pamoja na kutoa vitendea kazi ili kujua namna ya
upimaji na udhibiti.
0 comments:
Chapisha Maoni