Jumatano, Mei 21, 2014

TAREHE YA LEO KATIKA HISTORIA

Miaka 129 iliyopita katika siku kama hii mwaka 1885 aliaga dunia Victor Hugo mwandishi na malenga mashuhuri wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 83. Hugo alikuwa muungaji mkono mkuu wa mabadiliko kwa maslahi ya matabaka ya wanyonge na masikini nchini humo. Victor Hugo alijitumbukiza kwenye uwanja wa kisiasa akiwa na miaka 25 na kufanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge. Lakini ulipofika wakati wa utawala wa Napoleon wa Tatu alijiengua kwenye uwanja wa kisiasa na kubaidishwa kwa muda wa miaka 20 baada ya kupinga siasa za dikteta Napoleon wa Tatu.


Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita yaani mwaka 1912 alizaliwa Herbert Charles Brown mwanakemia wa Uingereza. Brown alizaliwa mwaka 1912 mjini London na familia yake ikahamia Marekani kabla hata hajatimu miaka miwili. Alijiunga na chuo kikuu cha Chicago mwaka 1935 na kusomea kozi ya Kemia na kuendelea na masomo hadi alipofanikiwa kuwa mhazili wa chuo kikuu. Mwaka 1979 alitunukia tunzo ya Nobel katika taaluma ya Kemia kutokana na jitihada alizofanya katika ugunduzi wa michanganyiko mipya ya Kemia Kaboni au Organic Chemistry. Herbert Charles Brown alifariki dunia mwaka 2004.


Na Miaka 34 iliyopita siku kama ya leo sawia na tarehe Mosi Khordad mwaka 1359 Hijria Shamsiya ulianza mzingiro wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, Marekani ilipoteza maslahi yake haramu nchini Iran. Kwa hivyo ili kuwaweka wananchi Waislamu wa Iran katika mashinikizo na kuulazimu mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usalimu amri, Marekani ilianzisha mzingiro dhidi ya Iran. Kufuatia uamuzi huo wa Marekani, Hayati Hadhrat Imam Khomeini (MA) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alitangaza kuwa uhai wa kiuchumi wa mataifa haufungamani na madola makubwa ya kibeberu. Akiwahutubia wananchi wa Iran, alisema: "Msiogope hata kidogo mzingiro hii wa kiuchumi kwani wakituwekea mzingiro wa kiuchumi tutaimarisha harakati zetu na hili litakuwa kwa maslahi yetu."

0 comments:

Chapisha Maoni