Kwa muda mrefu kumekuwapo na taarifa za watoto kupotea katika
mazingira tofauti, huku baadhi yao wakipatikana na kuunganishwa tena na
wazazi wao, lakini wengine hawajaonekana hadi leo.
Wakati wazazi na walezi wa watoto hao wakiwa
katika kiza kinene wasijue nini cha kufanya, serikali na wadau
wanaoshughulikia masuala ya watoto bado hawajapata jibu la swali; watoto
hao wapo wapi? Badala yake wameweka wazi sababu za watoto kupotea au
kuibwa.
Uchunguzi uliofanywa katika mikoa
mbalimbali nchini kubaini sababu za watoto hao kupotea, umebaini kuwa
baadhi ya watoto huondoka nyumbani baada ya kutokea ugomvi kati ya
wazazi au walezi wao.
Sababu nyingine ni kuibuka kwa biashara ya watoto
wanaouzwa kwa watu ambao hawana watoto, nchini na nje ya nchi na imani
za kishirikina zinazochochewa na waganga wa jadi.
Taarifa kutoka polisi zinasema kuwa baadhi ya
watoto walioripotiwa kwenye vituo vya polisi kupotea au kuibwa,
walibainika kuchukuliwa na mmoja wa wazazi wa mtoto kutokana na migogoro
kwenye familia.
Zaidi ya watoto 61 waliripotiwa kuibwa Dar es Salaam katika ya mwaka 2012 na 2013, kati yao wa kiume 28 na wa kike 32.
Taarifa kutoka Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam inaeleza kuwa mwaka 2012 kulikuwa na kesi 29 za wizi wa watoto,
ambapo kati yake watoto wanne wa kiume waliibwa hospitalini na watano wa
kike walichukuliwa wakiwa nyumbani. Watoto saba pekee kati ya wote
walioibwa ndiyo walipatikana.
Mwaka jana kulikuwa na kesi za wizi wa watoto 31,
kati yao wa kiume wawili walichukuliwa na watu wasiofahamika wakiwa
hospitalini na 17 wakiwa nyumbani. Pia watoto wa kike 12 walipotea mwaka
huo. Hadi kufikia Desemba 2013, watoto 21 walikuwa wamepatikana, ambapo
kati yao wa kiume 11 na wa kike 10.
Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Camillius Wambura
anasema watoto wachanga ndio wanaoibwa huku wenye umri mkubwa kidogo
hupotea kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo uzembe wa wazazi. Wambura
anasema baadhi ya wazazi waliiba watoto wachanga kwa sababu ya kutokuwa
na uwezo wa kuzaa, tabia iliyokomaa kutokana na wazazi wa aina hiyo
kushindwa kukubali hali waliyonayo.
Akitoa mfano anasema kuwa mama mmoja aliiba mtoto
mwenye umri wa wiki mbili Dar es Salaam, lakini alikamatwa siku chache
baadaye mkoani Rukwa.
Huyu mama alikuwa akiishi Rukwa, alimrubuni mume wake kuwa ana ujauzito, hivyo kwa kuwa siku za kujifungua zilikuwa zimefika alimwambia mumewe anataka kuja Dar es Salaam kujifungua kumbe alikuwa anakuja kuiba mtotoanasema.
Mama huyo alipomwiba mtoto alimpa rafiki yake
atangulie naye Morogoro ambapo alikwenda kumchukua na kwenda naye Rukwa,
hata hivyo mtoto huyo alifariki dunia baadaye. Wambura anazitaja sababu
za watoto kupotea kuwa ni pamoja na watoto kutoroka nyumbani baada ya
kukithiri kwa migogoro kwenye ndoa na wazazi kutokujali watoto wao.
0 comments:
Chapisha Maoni