Alhamisi, Mei 01, 2014

NUSURA KIJANA AMMALIZE BABA YAKE MZAZI

Katika tukio la kushangaza, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Anord Michael mkazi wa Mwenge jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita alifanya vurugu kubwa nyumbani kwao, akidaiwa kutaka kumuua baba yake mzazi kwa sababu ambazo hazikueleweka sawasawa.
Huku majirani na watu wengine wakishangazwa na kitendo hicho, Anord alimfungia ndani baba yake mzazi na kuanza kumshambulia kwa silaha mbalimbali kabla ya kuchukua panga kwa lengo la kutaka kummaliza kabisa.
Mzazi aliyenusurika kuuawa
Mzee Michael, kuona kijana wake amepania kummaliza, alipiga mayowe ya kuomba msaada, kitu ambacho kilifanikiwa kwani mara moja wasamaria wema walijitokeza na kumuokoa kwa kumhifadhi katika chumba kingine ndani ya nyumba hiyo.
Pamoja na hivyo, kijana huyo ambaye bado watu wana mashaka na utimamu wa akili yake, aliendelea kufanya fujo huku akivunja mlango wa chumba alichohifadhiwa baba yake ili aweze kumtoa roho, huku pia akitishia kumuua mtu yeyote ambaye angejaribu kumsogelea.
Kijana Arnold Michael aliyedhamiria kummaliza baba yake baada ya kudhibitiwa na polisi
Akiwa katika hatua za mwisho kuvunja mlango huo huku baba yake naye akianza kusali sala ya mwisho kabla ya mauti kumfika, ghafla askari wenye silaha waliwasili eneo hilo na kuanza kumdhibiti kijana huyo.
Hata hivyo, zoezi la kumdhibiti kijana huyo halikuwa rahisi, kwani bado alisababisha timbwili kubwa kabla ya maafande hao kutumia ujuzi wa kikazi bila kutumia risasi na kumweka chini ya ulinzi.
Katika hali ya kushangaza, baada ya askari polisi kumuuliza sababu iliyomfanya afikie uamuzi wa kumuua baba yake mzazi, Anord alidai mzee huyo ndiye chanzo cha yeye kuharibikiwa kimaisha.
Baadaye maafande hao walimzoa kijana huyo na baba yake kuelekea Kituo cha Polisi Mabatini  Kijitonyama  kwa mahojiano zaidi.

0 comments:

Chapisha Maoni