Hofu kubwa ilitanda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jumatatu ya wiki
iliyopita, baada ya Njiwa mweusi, mwenye miguu myekundu akiwa na hirizi
iliyofungwa katika mojawapo ya mabawa yake, kutua katika miguu ya
mgonjwa aliyekuwa amelazwa wodi namba tatu, jengo la Mwaisela.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya wauguzi wa wodi hiyo
ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini, walisema tukio hilo
lilitokea saa 3.55 asubuhi ambapo njiwa huyo aliingia kupitia dirishani
na kwenda kutua mguuni mwa Mwanahawa Ngunda (61) aliyekuwa amelala
kitanda namba 7, ambaye anadaiwa kuwa mkazi wa Kimara.
Njiwa huyo aliingia dirishani muda mfupi baada ya mgonjwa aliyekuwa
jirani na Mwanahawa, aitwaye Fatuma Musa (45) kurejea wodini hapo
akitokea kupata vipimo ambapo alisaidiwa na ndugu zake kupanda kitandani
kutokana na kuishiwa nguvu.
Inadaiwa kuwa baada ya kuingia wodini, njiwa huyo alianza kuzunguka
na kuleta taharuki kubwa kwa wagonjwa, wauguzi na ndugu waliokuwemo,
kiasi cha baadhi yao kukimbia huku wakipiga mayowe, kabla ndege huyo
hajaenda kutua miguuni mwa mgonjwa huyo, huku akiwa ametuna na macho
yake mekundu yakiwa yanalenga lenga machozi.
Inasemekena baada ya muda, ndege huyo aliruka na kutua dirisha
lililokuwa usawa wa kitanda alicholala Fatuma na kuzidi kuwakoroga watu
ambao waliamini kuwa ni mambo ya kishirikina. Ndugu wa mgonjwa
aliyetuliwa na njiwa huyo, anayedaiwa kuwa ni mama yake mzazi, alikosa
amani akiamini jambo baya lingemtokea.
Lakini katika hali ya kushangaza zaidi, mhudumu mmoja wa wodi hiyo
alisema wakati watu wakitaka njiwa huyo aondolewe ili kuondoa usumbufu,
dada wa Fatuma, aliyejulikana kwa jina la Mwanaisha Musa alimwambia
mhudumu kuwa yeye amempenda ndege huyo na anaomba apewe kwani anahitaji
kwenda kumfuga.
Mhudumu huyo alimweleza dada huyo kuwa anaweza kumchukua kama
anaweza, ndipo dada huyo alipomwambia kaka yake aliyetajwa kwa jina la
Yasini amkamatie, ambaye alimfuata dirishani na kumkamata bila ndege
huyo kuleta ubishi na kumkabidhi dada yake.
Baada ya dada huyo kukabidhiwa ndege huyo na yeye kumfunika na kanga
yake kama kichanga, ndipo ndugu wa mgonjwa aliyetuliwa na njiwa huyo
alipodaiwa kupandisha mashetani, akimfuata Mwanaisha ambaye alishaanza
kutoka wodini hapo.
Ndugu huyo alimfuata akidai kulikuwa na jambo kwani haiwezekani watu wote wamuogope njiwa huyo, lakini yeye amchukue bila hofu.
Inadaiwa kwamba pamoja na mtoto wa marehemu kupiga mayowe lakini
Mwanaisha hakuweza kumwachia njiwa huyo. Hata hivyo, mkusanyiko mkubwa
wa watu na mayowe, yaliwafanya walinzi kuingilia kati kumtaka mama
aliyemchukua njiwa huyo, kumkabidhi kwao mara moja.
Baada ya kukabidhi, Mwanaisha na kaka yake waliondoka na kumuacha
ndugu wa mgonjwa akilalamika juu ya usalama wa mama yake, hivyo kuanza
kuwapigia simu ndugu na jamaa zake akiwaeleza juu ya tukio hilo.
Mwandishi wa habari hizi alifika katika wodi hiyo na kukuta kitanda
alicholazwa mgonjwa aliyekanyagwa na njiwa akiwa hayupo na alipouliza,
wauguzi walisema mgonjwa huyo alifariki siku iliyofuata (Jumanne wiki
iliyopita) muda kama uleule wa saa 3.55 ambao njiwa huyo alifika.
Fatuma ambaye bado amelazwa wodini hapo alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikiri kutokea.
Ni kweli njiwa mwenye hirizi alitokea hapa wodini na alipoingia akamkanyaga mgomjwa mwenzangu, hata hivyo dada yangu alimpenda,
alimuomba mhudumu amruhusu amchukue, alikubaliwa na alipomchukua ndipo mtoto wa marehemu alipandisha mashetani na dada aliamua kuwakabidhi askari
alisema mgonjwa huyo aliyedai hali yake bado siyo
nzuri na kwamba anasubiri vipimo.
Habari zaidi zinasema njiwa huyo alitoweka kiaina kutoka mikononi mwa
askari wa Muhimbili wakati akishikiliwa katika ofisi kuu ya usalama
wakisubiri agizo kutoka kwa viongozi wa juu.
Msemaji mkuu wa hospitali hiyo, Aminiel Akaesha alipohojiwa alikiri
kutokea kwa tukio hilo huku baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo
wakizungumzia kuhusu uwepo wa ishara ya mambo ya kishirikina wakati
mwingine watu wasioonekana wakizungumza hasa katika eneo la chumba cha
kuhifadhia maiti.
0 comments:
Chapisha Maoni