Jumatatu, Mei 12, 2014

MWAMBUSI NDIYE KIBOKO YA MAKOCHA WAZUNGU

ZITAZAME timu sita zilizoshika nafasi za juu katika msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, zote zinafundishwa na makocha kutoka nje ya Tanzania lakini moja tu inafundishwa na mzawa.
Kocha Juma Mwambusi ndiye kocha pekee Mtanzania aliyeweza kushika nafasi ya tatu katika msimu uliopita akiwapiku makocha wengine watatu kutoka nje ya Tanzania. Ushujaa wa kipekee.
Mwambusi anaifundisha Mbeya City aliyoipandisha daraja kutoka Ligi Daraja la Kwanza na moja kwa moja ikaingia katika upinzani wa hali ya juu na timu kongwe za Ligi Kuu, kutokana na kasi yake, klabu hiyo ya Mbeya ingeweza hata kutwaa ubingwa.
Azam iliyotwaa ubingwa inafundishwa na Joseph Omog raia wa Cameroon, Yanga iliyoshika nafasi ya pili ilikuwa chini ya Hans Pluijm, ikafuata Mbeya City ya Mwambusi, Simba iliyoshika nafasi ya nne ilikuwa chini ya Zdravko Logarusic wa Croatia.
Nafasi ya nne ilichukuliwa na Kagera Sugar ya Kagera ikiwa chini ya Jackson Mayanja mwanasoka wa zamani wa Uganda na nafasi ya sita ilichukuliwa na Ruvu Shooting iliyo chini ya Tom Olaba raia wa Kenya aliyewahi kuifundisha timu ya Taifa ya nchi hiyo, Harambee Stars.
Mwambusi aliweza kupambana katikati ya vigogo vya soka nchini kwa soka safi na la ushindani lililokuwa likichezwa na vijana wake aliotoka nao daraja la kwanza ambao waliishia na kupambana pamoja uwanjani kuanzia mwanzo hadi mwisho wa ligi.
Hakuna ubishi, Mwambusi ameongeza idadi ya mashabiki katika Uwanja wa Sokoine Mbeya mara Mbeya City inapocheza na sasa viongozi wa timu zinazocheza na Mbeya City uwanjani hapo wanalalamikia kudhulumiwa mapato.
Nyuma ya mafanikio ya timu hii inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Mwambusi ndiye kila kitu.

0 comments:

Chapisha Maoni