Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
amesisitiza azma ya serikali ya Iran ya kuimarisha mahusiano ya pande
zote na nchi za Kiafrika bila ya kizuizi chochote. Dakta Muhammad Javad
Zarif aliyasema hayo jana usiku kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 51
ya kuasisiwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika OAU zilizofanyika mjini
Tehran.
Kwenye sherehe hizo, Dakta Zarif aliongeza kuwa, umoja huo
ulikuwa nembo ya uhuru kwa nchi zote za Kiafrika. Kwenye hotuba yake,
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran aliwakumbuka na kuwashukuru
viongozi wa zamani wa bara la Afrika kutokana na juhudi zao za kuleta
usawa na uhuru barani Afrika. Dakta Zarif ameelezea kuwepo ubaguzi na
ukoloni mamboleo katika baadhi ya maeneo duniani, na kusisitiza kwamba
kuna haja ya kuwepo umoja na mshikamano wa kukabiliana na vitendo hivyo.
Kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amelaani
vikali vitendo vya kundi lenye misimamo mikali la Boko Haram nchini
Nigeria na kuongeza kuwa, lengo la kundi hilo la kigaidi ni kuchafua
taswira ya dini tukufu ya Kiislamu. Naye Muhammad Ahmad Kassule Balozi
wa Uganda mjini Tehran ameishukuru Iran kwa kuimarisha mashirikiano na
nchi za Kiafrika na kutaka juhudi zaidi zifanyike kwa lengo la
kuboreshwa mashirikiano hayo katika sekta binafsi kati ya Iran na bara
la Afrika. Sherehe hizo zilihudhuriwa na mabalozi wa nchi kadhaa za
kigeni walioko mjini Tehran na shakhsia mbalimbali wa Kiirani na kigeni
walioko hapa nchini. Aidha Waziri wa Sheria wa Uganda na Waziri wa
Uchukuzi wa Ivory Coast walikuwa wageni maalumu kwenye sherehe hizo.
0 comments:
Chapisha Maoni