Jumatano, Mei 14, 2014

BAADA YA ALBINO KUTENDEWA UNYAMA SIMIYU, SERIKALI IMEOMBWA WAGANGA WA KIENYEJI WAFUTIWE VIBALI

Polisi nchini Tanzania wamewakamata waganga wawili wa kienyeji baada ya mwanamke mmoja mwenye ulemavu wa ngozi au Abino kuuwawa kwa kuchinjwa.
Moja ya miguu yake pamoja na vidole vilinyofolewa baada ya shambulizi hilo la hapo jana Jumanne katika mkoa wa Simiyu Kaskazini Mashariki mwa Tanzania. Kumekuwa na visa vingi vya mauaji ya albino katika eneo hilo hapo awali.

Shirika la kutetea haki za watu wenye ulemavu wa ngozi Albino la 'Under the Same Sun limeiomba serikali ya nchi hiyo kufuta vibali na shughuli zote za waganga wa jadi kwa madai kuwa wao ndiyo chanzo cha kuuawa kwao.
Kuuawa kwa mwanamke Munghu Lugata mlemavu wa ngozi toka kijiji cha Gasuma mkoani Simiyu Kaskazini Magharibi mwa nchi hiyo kumeacha hisia na uchungu kwa walemavu wengine waliopata mikasa hiyo.
Akizungumza na mwandishi wa BBC Leonrad Mubali kwa uchungu na kilio, Mariamu Staford mlemavu wa ngozi Albino amesema kwamba tukio la kuuawa kwa Munghu Lugata mwanamke mwenye umri wa miaka 40 juzi linamkumbusha mkasa wake uliomkuta wa kukatwa mikono yake yote, zaidi ya miaka mitano iliyopita na sasa anatumia mikono ya bandia ya vyuma huku akisema malengo yake mengi yamekwama.
Albino wamekuwa wakihangaishwa sana nchini Tanzania ambako baadhi ya watu wanaamini kuwa dawa za miujiza zinazotengezwa kutokana na viungo vya miili yao zinaleta bahati nzuri.
Mashambulizi yamepungua katika siku za hivi karibuni lakini mauaji ya hivi punde yamepelekea shirika moja la kutetea haki za Albino kutoa wito kwa serikali kupiga marufuku waganga wote wa kienyeji.
Matukio mengi ya maujia ya walemavu nchini Tanzania yamekuwa yakihusishwa na imani za kishirikina huku waganga wa jadi wakihusishwa.
Mkoa wa Simiyu ni moja katika maeneo kaskazini magharibi mwa Tanzania yenye matukio mengi ya mauaji hayo.
Hivi karibuni nchini Tanzania umezinduliwa mnara maalumu unaoitwa NITHAMINI, mnara pekee duniani unaowakilisha kupinga mauaji ya albino huku Tanzania ikiwa ni moja ya nchi yenye matukio mengi ya ukatili dhidi ya walemavu hao

0 comments:

Chapisha Maoni