Wamiliki wa magari ya Toyota nchini wametakiwa kuhakiki magari
yao na kuyarejesha kwa uchunguzi yale yatakayobainika kuwa na hitilafu
za kiufundi katika mfumo wa baadhi ya vifaa vyake.
Taarifa ya Toyota Tanzania kwenye vyombo vya
habari ilieleza jana kwamba magari yanayohusika ni RAV 4, Hilux na
Fortuner yaliyotengenezwa kati ya mwaka 2006 na 2010.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa
Toyota Tanzania, Yusuph Karimjee kueleza mwishoni mwa wiki iliyopita
kwamba ofisi yake inafanya tathmini baada ya kampuni hiyo yenye makao
yake Japan, kuamua kurejesha magari hayo baada ya kubaini matatizo ya
kiufundi.
Imesema wamiliki watakaohakiki magari yao na
kubaini hitilafu, yatafanyiwa matengenezo bure Dar es Salaam, chini ya
wataalamu wake.
Taarifa hiyo ilisema wateja wote watakaobaini hitilafu katika magari hao wataarifiwa jinsi ya kupatiwa huduma hiyo.
Hatua hiyo inatokana na kubainika kwa matatizo
katika nyaya zilizounganishwa na mifuko ya hewa kwa ajili ya kuokoa
maisha wakati wa ajali, kwenye magari hayo.
Kutokana na muundo na eneo ulipowekwa mfumo wa
nyaya zinazoendesha mifuko ya hewa, hasa upande wa dereva, imeelezwa
kwamba kunaweza kuwa na athari iwapo usukani utapata hitilafu wakati wa
ajali.
Iwapo mfumo huo utaathiriwa, taa ya tahadhari
inaweza kuwaka na kuathiri mfuko huo kwa upande wa dereva na kuufanya
ushindwe kufanya kazi kama ilivyopangwa.
Hata hivyo, kampuni hiyo ilisema katika taarifa
yake kuwa haijapokea taarifa ya ajali yoyote duniani iliyotokana na
hitilafu hiyo.
0 comments:
Chapisha Maoni