Serikali ya Kenya imewatimua wakimbizi 82 kutoka Somalia ambao walikuwa
nchini humo kinyume cha sheria. Waziri wa Mambo ya Ndani Kenya Joseph
Ole Lenku amesema Wasomali hao wamerejeshwa Mogadishu na kwamba
wahamiaji haramu wapatao 472 bado wanashikiliwa na polisi kufuatia
oparesheni ya hivi karibuni ya usalama nchini humo. Ole Lenku amesema
sheria imefuatwa katika oparesheni hiyo kwani Wasomali wote
waliotimuliwa wamepelekwa Mogadishu leo asubuhi wakiwa wameandamana na
Balozi wa Somalia nchini Kenya. Hapo jana Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR lilielezea wasi wasi wake kuhusu kutiwa
mbaroni idadi kubwa ya wakimbizi Wasomali katika mji mkuu wa Kenya,
Nairobi. Katika taarifa, UNHCR ilisema wakimbizi Wasomali wanaoshikiliwa
wanapaswa kulindwa na kutokamatwa kiholela. Waziri wa Mambo ya Ndani wa
Kenya Joseph Ole Lenku amenukuliwa akisema zaidi ya watu 4,000
wamekamatwa katika siku za hivi karibuni. Vikosi vya usalama Kenya
vinatekeleza oparesheni kubwa ya kiusalama yenye lengo la kuwasaka
magaidi kufuatia hujuma za kigaidi katika miji ya Nairobi na Mombasa.
Kundi la kigaidi la Al Shabab limenukuliwa mara kadhaa likisema
litatekeleza hujuma Kenya kulipiza kisasi uingiliaji wa jeshi la Kenya
nchini Somalia.
0 comments:
Chapisha Maoni