Watu 10 wamekufa papo hapo na mwingine kupoteza maisha alipokuwa
akipelekwa hospitali baada ya basi walilokuwa wakisafiria kupata ajali
mkoani Simiyu.
Ajali hiyo ilitokea eneo la Itwilima A, Kata ya
Kilorei, Wilaya ya Busega baada ya basi hilo la Luheye lifanyalo safari
zake kati ya Bunda na Mwanza kupata hitilafu na kugonga mti na baadaye
nyumba.
Akizungumza katika Hospitali ya Wilaya ya Magu
jana, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Pascal Mabiti alisema watu waliokufa ni 11
na majeruhi 44.
Mabiti alisema mtu mmoja aliyefariki wakati
akipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jina lake bado lina
utata... “Jina la huyu mama ambaye ameacha watoto watatu; Joyce Wilson
(6), Jenipher Wilson (3) na Jack (miezi miwili), wametwambia mama yao
alikuwa anaitwa Lucia Wilson, lakini taarifa tulizopata kutoka Bugando
zinasema alikuwa anaitwa Fodia Guniniga.”
Alisema majeruhi 19 ni wanawake na 25 wanaume na
kwamba, wachache wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu lakini
wengi walipelekwa Bugando kutokana na hali zao kuwa mbaya. “Natoa wito
kwa wananchi kwenda Hospitali ya Bugando Mwanza kutambua maiti. Miili ya
watu wote waliokufa tumeihifadhi hapo na hakuna aliyetambuliwa zaidi ya
huyo mama ambaye ameacha watoto watatu,” alisema.
Shuhuda wa ajali hiyo, Paulina Ruge (57) ambaye ni
mmiliki wa nyumba iliyogongwa na basi hilo, alisema ilitokea kati ya
saa 4:30 na 5:00 asubuhi.
Alisema baada ya ajali alishuhudia ikitolewa miili ya watu 10 waliokufa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo
alisema baada ya kutokea ajali hiyo dereva ambaye jina lake
halijafahamika alikimbia na polisi wanaendelea kumtafuta.
0 comments:
Chapisha Maoni