Jumatano, Aprili 30, 2014

MAMA WA MTOTO ALIYEKUFA AKIOGELEA LANDMARK HOTEL ATOA MSAMAHA

Devotha Mbutwa, mama wa mtoto Janeth Kihoko, aliyekufa wakati akiogelea na wenzake, amemsamehe mzazi wenzake aliyemchukua mwananye kwenda kwenye hoteli ambayo mauti ilimkuta.

Janeth alifariki dunia pamoja na watoto wengine wawili katika Hoteli ya Landmark, Mbezi Beach walikokwenda kusherehekea siku ya kuzaliwa mtoto wa jirani yao.

Mbutwa alisema amechukua uamuzi huo kwa sababu yeye ni Mkristo na kwamba tukio hilo halikudhamiriwa.

Alisema kuwa hakupata taarifa kutoka kwa jirani yake, Anita Mboka kuwa angewachukua watoto hao kwenda kwenye sherehe, lakini watoto ndiyo waliompa taarifa tangu siku ya Pasaka.

Alisema alikuwa akikumbushwa na watoto wake Janeth na Goodluck kuwa walialikwa kwenye sherehe ya kuzaliwa na jirani yao na kwamba wangekwenda baharini kuogelea, lakini aliwakataza.

Alipoona wanasisitiza, aliamua kuwaruhusu, lakini kwa sharti la kutoogelea baharini.

“Ilipofika jioni, Jumapili kama kawaida nikampigia simu mwanangu Goodluck kumuuliza kama wako nyumbani, akaniambia kuna tatizo limetokea, Janeth ameangukia kwenye bwawa la kuogelea,” alisema Mbutwa huku akilia kwa uchungu.

Mbutwa anasema alipofika nyumbani kwa jirani yake Mboka, alipewa namba zake za simu akampigia ili kujua kilichokuwa kikiendelea.

Anasema kuwa baadaye alifika jirani yake Anita Mbuta na kumwomba msamaha kuhusu yote yaliyotokea kwa mtoto wake na kumuahidi kuwa pamoja naye na kumsaidia kikamilifu kwenye mazishi.

0 comments:

Chapisha Maoni