Mwenyekiti wa Muda wa Bunge la Katiba, Pandu Ameir Kificho
amekiri kuwasilisha waraka kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa
chini ya Jaji Joseph Warioba na kupendekeza Zanzibar na Tanganyika kuwa
na mamlaka huru, hatua ambayo imezua malalamiko miongoni mwa makada wa
chama hicho ambao wamesema huo ni usaliti.
Akizungumza kwa simu kutoka Dodoma, Kificho ambaye
pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), alisema kimsingi
waraka huo ulilenga kuipa nguvu Zanzibar kushughulikia mambo yasiyo ya
Muungano ili kujiimarisha kiuchumi.
Kauli ya Kificho inakuja wakati baadhi ya wajumbe
wa CCM kutoka Zanzibar wakiitisha mkutano na kutoa tamko la kumshutumu
kwa kutoa mapendekezo hayo, wakisema ni kinyume na msimamo wa chama
hicho.
Kificho alionyesha kushangazwa na madai kuwa mapendekezo hayo yaliyoandaliwa na watu wanne ambayo ameyasaini si msimamo wa BLW.
“Tatizo lililopo ni tafsiri ya kila mmoja
anapousoma waraka huo, hakuna sehemu tuliyoandika tunataka Serikali
tatu, mamlaka huru maana yake kila upande uwe na uwezo wa kushughulikia
mambo yake yasiyo ya Muungano na kujijenga kiuchumi, ikiwa ni pamoja
Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu ya Kimataifa (OIC) na siyo
kuunda dola,” alifafanua Spika Kificho.
Alisisitiza kuwa angependa mambo ambayo hayamo
katika orodha ya Muungano yaendeshwe na Zanzibar bila ya kuwekewa
vikwazo mahali popote.
Madai hayo ni dalili za wazi za mgawanyiko baina
ya wajumbe wa CCM ambao wameanza kuonyesha makundi mawili yenye misimamo
tofauti.
Kundi linalomshutumu Kificho, linawajumuisha
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Juma Ali Shamhuna, Waziri Kiongozi
mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Spika wa BWZ, Ali Abdallah Ali.
Jana, kundi hilo lilimtuhumu Kificho kuwa
hakuwashirikisha wenzake katika mapendekezo Serikali tatu
aliyoyawasilisha kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakisema Baraza la
Wawakilishi, kama taasisi, halikutoa msimamo wa pamoja.
Hata hivyo, mtazamo huo wa BLW unatofautiana na
ule wa Kificho uliowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya
Zanzibar, Othman Masoud Othman, ukipendekeza Serikali tatu.
“Kwa vile mfumo wa Serikali mbili uliopo sasa
hauwezi kujenga Muungano utakaohimili mabadiliko ya kisiasa na kwa vile
umejaribiwa na kuthibitishwa kuwa umeshindwa kujenga Muungano imara,
uachwe katika kuendesha Muungano wa Tanzania,” inasomeka sehemu ya
taarifa hiyo ya Othman.
Jana asubuhi, zaidi ya wajumbe 10 wa Baraza la
Wawakilishi akiwamo Shamhuna, Nahodha na Ali waliitisha mkutano wa
waandishi wa habari mjini Dodoma na kumtupia lawama Kificho wakisema;
“Amewasaliti katika mchakato huo wa Katiba.”



0 comments:
Chapisha Maoni