Jumatatu, Machi 17, 2014

SASA HII NDIO SIRI ILIYOFANYA MZOZO KUIBUKA BUNGENI JANA

Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa), walitangaza mapema jana kwamba wangepinga ratiba nzima kuendelea hadi madai yao ya kumtaka Rais Jakaya Kikwete afungue Bunge kwanza kabla ya rasimu kuwasilishwa yasikilizwe.
 
Madai ya Ukawa 
  
Viongozi wa Ukawa waliitisha mkutano wa wanahabari na kutangaza kususia kuendelea na ratiba wakipinga uvunjwaji wa kanuni unaodaiwa kufanywa na Sitta.
Katika uamuzi huo uliofikiwa jana mchana, mmoja wa viongozi wa Ukawa, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema: “Kwa sababu za ukiukwaji wa kanuni, tunapenda kueleza kwamba hatupo tayari kuunga mkono, tutapinga kwa kadri ya uwezo wetu, mambo makubwa manne kufanyika bungeni.”
Alisema mambo ambayo wanapinga ni uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba uliopangwa kufanyika jana kabla ya ufunguzi wa Bunge maalumu unaotarajiwa kufanywa na Rais Jakaya Kikwete.
Profesa Lipumba pia alisema wangepinga kufanyika kwa semina ambayo ilipangwa kuongozwa na wataalamu wa ndani au nje ya nchi leo kuhusu uzoefu katika masuala ya Bunge la Katiba.
“Pia tutapinga hotuba ya Rais endapo itatolewa baada ya uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba na pia jambo jingine lolote linalokiuka Kanuni za Bunge Maalumu,” alisema Profesa Lipumba aliyeambatana na wajumbe wenzake, James Mbatia na Tundu Lissu.
Kanuni zinazolalamikiwa
Profesa Lipumba alisema mara baada ya kuchaguliwa, Sitta amevunja Kanuni ya 7 (1) (g) na (h) ambazo zimeweka mpangilio wa shughuli zote za Bunge Maalumu.
“Hotuba ya ufunguzi ambayo itatolewa na Rais, ilielezwa wazi kwenye kanuni kuwa itatangulia na kufuatiwa na uwasilishaji wa Rasimu ya Katiba. Hivyo kwa kutangaza kuanza kuwasilisha rasimu ni kuvunja kanuni,” alisema.

0 comments:

Chapisha Maoni