Jumatatu, Machi 17, 2014

MISRI YABORESHA ULINZI

Serikali ya mpito ya Misri imeimarisha usalama kufuatia shambulizi lililofanywa kwenye kituo cha upekuzi cha kijeshi huko Cairo mji mkuu wa nchi hiyo.
Watu waliokuwa na silaha jana walikishambulia kituo kimoja cha upekuzi mjini Cairo na kuwauwa wanajeshi sita. Serikali ya mpito ya Misri kwa upande wake imeeleza kuwa imeamua kupambana na yeyote atakayejaribu kuwashambulia raia na maeneo ya serikali na kwamba mashambulizi dhidi ya jeshi yatashughulikiwa na mahakama za kijeshi.
Serikali hiyo ya mpito ya Misri imeongeza kuwa imeamua kuimarisha hali ya usalama nchini humo ili kuzuia wimbi la mashambulizi yaliyopelekea kuuliwa wanajeshi wasiopungua 300 tangu kuanza mashambulizi hayo baada ya kupinduliwa na jeshi mwezi Julai mwaka jana, Mohamed Morsi Rais wa kwanza kuwahi kuchaguliwa kidemokrasia huko Misri.
Jeshi la Misri limeinyoshea kidole cha tuhuma harakati ya Ikhwanul Muslimin na wafuasi wa Mohamed Morsi, hata hivyo ushahidi mdogo umetolewa kuweza kuyapa nguvu madai hayo. Ikhwanul Muslimin pia imekanusha kuhusika na mashambulizi hayo.

0 comments:

Chapisha Maoni