Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda, anayetumikia
kifungo cha miaka 18 gerezani kwa wizi wa fedha katika Akaunti ya
Madeni ya Nje (Epa) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), amelazwa katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akisumbuliwa na tatizo la mgongo.
Msemaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji
wa Mishipa ya Fahamu (MOI), Jumaa Almasi aliliambia Fichuo amesema
kuwa Maranda alifikishwa hospitalini hapo Februari 16, mwaka huu.
“Ni kweli Maranda yupo hapa tangu Februari 16 na
alifanyiwa upasuaji kutokana na matatizo ya mgongo wiki tatu zilizopita
na hali yake inaendelea vizuri ingawa hawezi kuamka kitandani,” alisema
Almasi.
Kuhusu ugonjwa unaomsumbua, Almasi alisema:
“Ugonjwa ni siri kati ya mgonjwa na daktari wake na binafsi siwezi
kuuelezea ila kama nilivyosema alifanyiwa upasuaji wiki tatu
zilizopita.”
Alisema Maranda yuko chini ya uangalizi wa askari Magereza kutokana na kuendelea kutumikia adhabu ya kifungo gerezani.
Maranda aliyewahi kuwa Mweka Hazina wa CCM mkoani
Kigoma na binamu yake, Farijala Hussein, ambao kwa pamoja walipatikana
na makosa sita kati ya saba waliyokuwa wanakabiliwa nayo ya kujipatia
Sh2.2 bilioni za Epa.
Maranda na wenzake pia wanatumikia kifungo cha
miaka mitatu jela ambayo itakwenda sanjari na kifungo cha awali cha
miaka mitano kutokana na kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa, ambayo
ni kula njama, kughushi nyaraka, kuwasilisha hati bandia na kujipatia
kiasi hicho cha fedha.
Novemba 2012, Maranda kwa mara ya tatu alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na kuamriwa kurejesha Sh616.4 milioni.


.jpg)

0 comments:
Chapisha Maoni