Mvua iliyoambatana na upepo mkali imeezua shule ya sekondari Kondoa
Islamic iliyoko wilayani Kondoa mkoani Dodoma na kusababisha wanafunzi
33 kukimbizwa hosipitali huku wengine zaidi ya 100 wakikosa mahala pa
kulala pamoja na kuharibu vitu mbalimbali ikiwemo vifaa vya kufundishia
na kujifunzia vyakula na malazi ya wanafunzi.
Chanzo kilifika eneo la shule na kushuhudia uharibifu
mkubwa uliofanywa na mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali ambapo
sehemu zilizoathirika kwa kiasi kikubwa ni pamoja na bweni la wasichana,
ukumbi wa kufanyia mitihani, madarasa pamoja na baadhi ya ofisi huku
baadhi ya wanafunzi wakionekana kuhaha kutafuta sehemu za kujistiri
kufuatia vitanda na matandiko yao kulowana na maji huku mvua ikiendelea
kuwanyeshea .
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Salum Athumani anasema
mvua hiyo imeathiri utendaji wa shule hiyo kwa kiasi kikubwa kutokana na
kusimamisha masomo ya wanafunzi huku akiwaomba wakazi wa wilaya hiyo
na wilaya za jirani kutoa msaada wa hali na mali kuhakikisha hali ya
shule hiyo inarejea kama ilivyokuwa awali.
Kufuatia janga hilo uongozi wa halmashauri ya
wilaya ya kondoa kupitia kamati ya maafa ya wilaya umechukua hatua za
dharura ikiwemo kupeleka vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kufanya ukarabati
ambapo mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya kondoa ezekiel mwalongo
amesema licha ya mvua hiyo kuleta madhara shuleni hapo lakini pia
imeezua zahanati ya kijiji cha Mkekena kata ya Itololo pamoja na nyumba
tatu za wakazi wa kijiji hicho.



0 comments:
Chapisha Maoni