Waziri wa Fedha, Saada Mkuya amekiri Serikali kuwa katika hali
ngumu, lakini akasema kuwa mkakati uliopo ni kudhibiti matumizi ili
yaendane na fedha iliyopo.
Waziri Saada alisema hayo kwa njia ya simu,
alipotakiwa na mwanahabari Jumapili kujibu madai ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Serikali (CAG) juu ya kauli yake ya hivi karibuni aliyoitoa
katika mkutano mjini Dodoma.
“Ni kweli nimesikia alichosema CAG na nadhani
alimaanisha kudhibiti matumizi ya rasilimali kulingana na mahitaji. Siyo
kwa Tanzania tu, nchi zote huwa zinazingatia matumizi ya rasilimali
kulingana na mahitaji yaliyopo” alisema Saada na kuongeza:
“Sisi kama wizara tumejipanga kukusanya na
kutegemea fedha zetu za ndani kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA).
Tunategemea misaada, lakini huwa inachelewa. Hata wakaguzi nao wanapaswa
kuangalia hilo.”
Hata hivyo, Saada alisema kuwa Serikali ina fedha za kutosha kuendesha shughuli zake.
Alhamisi wiki hii CAG,Ludovick Utoh akifungua
Mkutano wa pili wa Baraza la Wafanyakazi wa Ukaguzi nchini mjini Dodoma
alisema, Serikali ya Tanzania iko hoi kifedha hivyo Bunge na Serikali
lazima wajitathimini na kuongeza wanayo matumaini kutokana na ushauri
ambao umekuwa ukitolewa na ofisi yake kufanyiwa kazi.
0 comments:
Chapisha Maoni