Ijumaa, Januari 24, 2014

WATANZANIA WOTE SASA KUWA NA BIMA YA AFYA

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imesema imeandaa mpango wa kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanaingizwa kwenye mfumo wa malipo ya matibabu kupitia Bima ya Afya kwa lengo la kuboresha sekta hiyo nchini.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, wakati wa ziara yake ya kwanza baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo pia alikutana na uongozi wa Moi na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la MOI lenye ghorofa saba ambalo linatarajiwa kukamilika Mei mwaka huu.
Akizungumza katika kikao hicho baada ya kukagua jengo hilo, Dk. Seif Rashid, alisema serikali ina mpango wa kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanapatiwa matibabu kupitia mfumo wa bima ya afya.
“Bima ya afya ni lazima, maana tumezoea kusema tu bima ya gari lakini bima ya afya kwa mwanadamu ni ya lazima, iwapo Bunge likiridhia itatubidi tutengeneze sheria kwa ajili ya kulisimamia namna ya kuiendesha,” alifafanua Dk. Rashid na kuongeza:
“Tukiwa na sheria hiyo tutahakikisha Mtanzania anakuwa na bima ya afya, katika kufanikisha hili tutajaribu ‘kulink’ (kushirikiana) na watu wanaoshughulika na masuala ya bima na tukifanikiwa tutakuwa tumetatua matatizo mengi.”
Kuhusu madaktari wanaokwenda kuajiriwa nje ya nchi, Waziri Seif Rashid, alisema serikali imeshaandaa mkataba maalumu utakaowataka madaktari wanaohitimu masomo yao katika vyuo vya hapa nchini kufanya kazi nchini.
Pia, aliwataka madaktari wote kutoka maeneo mbalimbali nchini ambao bado hawajaajiriwa kupeleka maombi ya ajira serikalini ili waweze kuajiriwa kwani sekta hiyo ina upungufu mkubwa wa wataalamu na kwamba inazidi kukua.

Dk. Rashid alisema kati ya mwaka 2005 na 2006, kulikuwa na upungufu wa watumishi wa afya kwa asilimia 67, na sasa upungufu uliopo ni asilimia 49.
Katika kufanikisha hilo, Waziri Rashid, aliitaka taasisi hiyo kuhakikisha inatumia mifumo ya teknolojia ya kisasa kuboresha utoaji wa huduma za afya na kwa jinsi hiyo kuongeza pato lake.
Jengo hilo litakuwa na jumla ya vitanda 200 na litasaidia kupunguza msongamano.

0 comments:

Chapisha Maoni