Jumanne, Januari 28, 2014

WANAFUNZI NA WAALIMU WA SHULE ZA SEKONDARI NCHINI KUPATA TABLET


Serikali inakusudia kutoa maelfu kwa maelfu ya tabuleti za kufundishia masomo mbalimbali kwa wanafunzi na walimu wa shule za sekondari nchini kama njia ya ubunifu zaidi, ya kisayansi na ya uhakika ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT).
Ili kufanikisha mpango huo, Serikali inakusudia kuingia ushirikiano na taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Opportunity Education Trust ya Marekani ambayo jana ilizindua mpango wa majaribio wa utoaji wa tabuleti hizo kwa wanafunzi na walimu wao wa shule za sekondari nchini.
Mpango wa Serikali wa kusambaza tabuleti kwa wanafunzi na walimu wa shule za sekondari ulitangazwa juzi na Rais Jakaya Kikwete, alipokutana na kuzungumza na Joe Ricketts, mwenye taasisi ya Opportunity Education Trust na mmoja wa matajiri wa Marekani. Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete alimweleza kwa undani Ricketts hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali yake kupania na kuboresha elimu tokea mwaka 2006, hatua ambazo zimechangia kupanua kwa kasi na kwa kiwango kikubwa wigo wa utoaji elimu nchini na changamoto ambazo zimezuka kutokana na upanuzi huo mkubwa.

Rais Kikwete alisema baadhi ya changamoto hizo ni ukosefu wa walimu na hasa wa masomo ya sayansi na ukosefu wa vitabu vya kufundishia, changamoto mbili kubwa ambazo zinatatuliwa na matumizi ya tabuleti. “Mbali na upanuzi mkubwa wa nafasi za wanafunzi kupata elimu ya ngazi mbalimbali, pia tumepanua sana ufundishaji wa walimu. Mwaka 2005, vyuo vyetu vyote vilikuwa vinatoa walimu 500 sasa tunatoa walimu 12,000 kwa mwaka. Hivyo, tunaamini kuwa katika mwaka mmoja ama miwili ijayo, tutakuwa tumemaliza tatizo la walimu wa masomo ya sanaa,” alisema. Hata hivyo, alisema bado nchi inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi. "Tuna upungufu wa walimu 26,000 na kwa mwaka vyuo vyetu vyote vinahitimisha walimu 2,100 tu," alisema. Chini ya mpango huo wa majaribio wa kusambaza teknolojia hiyo ya kisasa, taasisi ya Opportunity Education Trust inatoa tabuleti 1,100 kwa ajili ya walimu na wanafunzi wa sekondari katika shule 33. Ricketts alimwambia Rais Kikwete: “Hapa tunafanya majaribio na Tanzania ni nchi ya kwanza duniani miongoni mwa nchi ambazo tunaunga mkono mipango ya maendeleo kunufaika na mpango huo wa majaribio. Ni azma yetu kuwa baada ya kuwa tumefanya tathmini ya mafanikio na changamoto za hatua hii ya majaribio, tutaupanua mpango huu kushirikisha shule nyingi zaidi kwa kushirikiana na Serikali kwenye mpango wake mkubwa wa kusambaza teknolojia hii katika shule zote za sekondari hapa Tanzania.” Ricketts na wataalam wake pamoja na maofisa wa Serikali walianza kutekeleza mpango huo jana kwa kutoa tabuleti kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Wama Nakayama iliyoko mkoani Pwani. Baada ya hapo, shughuli hiyo itahamia Zanzibar na Pemba, kabla ya Ricketts na wataalam wake kutoa tabuleti kwa shule zilizoko mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Kagera na Morogoro. Shule zinazonufaika katika mpango huo ni za Serikali na binafsi na kwa kuanzia masomo ambayo yanapatikana katika tabuleti hizo ni Hesabu, Jiografia, Historia na Kiingereza.

0 comments:

Chapisha Maoni