Ijumaa, Januari 24, 2014

RAIS KIKWETE APATA MWALIKO WA KWENDA NIGERIA

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria wakati viongozi hao wawili walipokutana na kufanya mazungumzo Alhamisi, Januari 23, 2014, kwenye Hoteli ya Intercontinental, Davos, Uswisi, ambako  walikuwa wakihudhuria  Mkutano wa Mwaka huu wa Taasisi ya Uchumi Duniani –WEF.
RAIS KIKWETE AALIKWA NIGERIA NA RAIS JONATHAN
Rais wa Nigeria Mheshimiwa Goodluck Jonathan amemwalika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuhudhuria Mkutano wa Taasisi ya Uchumi Duniani Afrika (WEF-Africa) unaofanyika katika mji mkuu wa Nigeria wa Abuja mwezi Mei mwaka huu.
Rais Jonathan ametoa mwaliko huo kwa Rais Kikwete wakati viongozi hao wawili walipokutana na kufanya mazungumzo leo, Alhamisi, Januari 23, 2014, kwenye Hoteli ya Intercontinental, Davos, Uswisi, ambako viongozi hao wanahudhuria wa Mkutano wa Mwaka huu wa Taasisi ya Uchumi Duniani –WEF.
Rais Kikwete amekubali mwaliko huo wa kuhudhuria Mkutano huo uliopangwa kufanyika Mei 7-9 mwaka huu mjini Abuja, Nigeria.   
Mkutano huo kati ya viongozi hao wawili umehudhuriwa na Mawaziri wa Nigeria wa Mambo ya Nje na Fedha na Uchumi.
Nigeria inakuwa nchi ya nne katika Afrika kuandaa mkutano huo. Kwa miaka mingi, mkutano huo wa WEF-Africa ulikuwa unafanyika Cape Town, Afrika Kusini mpaka Tanzania ilipofanikiwa kuwa nchi ya kwanza ya Afrika nje ya Afrika Kusini kuandaa Mkutano huo mwaka 2010.
Tokea wakati huo, Ethiopia imeandaa mkutano huo na sasa Nigeria.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 Januari, 2014

0 comments:

Chapisha Maoni