MTANGAZAJI wa Runinga ya Channel Ten, Penniel Mungilwa ‘Penny’
amefunguka kuwa sifa ya aliyekuwa mpenzi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond’ ni
kama chizichizi lakini kwa undani zaidi ni mtu makini.
Penny alifunguka hayo mbele ya kinasa sauti cha Ijumaa Wikienda hivi
karibuni ambapo mbali na kutamka kauli hiyo, alifunguka mambo mengi
yaliyohusu penzi lao ambalo alilitaja kuwa wamelipumzisha kwa kupeana
nafasi.
Akizungumzia sifa za staa huyo aliyeogelea naye penzini kwa kipindi
cha mwaka mmoja na ushee hivi, Penny alisema watu wote wanamjua Diamond
ni kama chizichizi vile kutokana na mapepe anayoyafanya akiwa mzigoni
lakini linapokuja suala la uhusiano, anakuwa makini sana.
“Diamond ni kama chizichizi vile lakini kwa ndani ni mtu makini sana.
Anajua kulea, anajua umuhimu wa mapenzi na anaelewa anatakiwa kumfanyia
nini mpenzi wake anapokuwa nyumbani, anajali,” alisema Penny na
kuongeza:
“Watu wamuanavyo nje na jinsi alivyo katika maisha ya kawaida ni
tofauti kabisa, mapepe anayafanya anapokuwa jukwaani na sehemu nyingine
zinazohusu kazi yake na si nyumbani.”
Katika aya nyingine, Penny alitiririka na mistari kuwa, baada ya
kuona penzi lao limetawaliwa na misukosuko, walikaa chini kwa pamoja na
kuamua kupeana nafasi ya kila mmoja wao kufanya mambo yake, hakuna kati
yao aliyemtamkia mwenzake kuwa sikutaki.
Alisema katika maisha huwa hapendi vitu vya kuambiwa, hata aliposikia
taarifa za Diamond kurudiana na Wema kwa mara ya kwanza nchini China,
hakuamini hadi walipokuja kukaa naye na kuzungumza ndipo walipoamua
kupeana nafasi.
Hata hivyo, Penny alisema anaamini kuwa Diamond amerudiana na Wema
lakini yeye kwa sasa ‘bado yupoyupo sana’, akakiri kuwa anatongozwa na
watu tofauti na endapo ikitokea akaamua kuanzisha uhusiano mpya,
hatahitaji mtu maarufu kwani anahitaji maisha yake kuwa ya siri, tofauti
na zamani.
0 comments:
Chapisha Maoni