Siku ya Alhamisi, mpatanishi wa Umoja wa Mataifa Lakhdar Brahimi,
alifanya mashauriano ya pande hizo mbili ili kutathmini ikiwa wako
tayari kufanya mazungumzo ya pamoja.
Uswizi ilikuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo kwa siku ya kwanza mjini
Montreux, ambapo wajumbe wa pande hizo mbili walirushiana maneno makali.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa zaidi ya watu laki moja wameuawa nchini Syria Tangu mzozo huo kuanza miaka mitatu iliyopita.
Mapigano hayo pia yamesababisha zaidi ya watu milioni tisa nukta tano
kuhama kutoka makwao, hali iliyosababisha mzozo mkubwa wa kibinadam
ndani ya nchi hiyo na pia katika nchi jirani.
Brahimi alifanya mazungumzo tofauti ya faragha na wawakilishi wa rais Bashar al-Assad na wale wa baraza la mpito.
Mzungumzo hayo hayakutarajiwa kwa kuwa pande hizo mbili hazikuwa zimekutana kufanya mashauriano yoyote rasmi.
Mabalozi wa mataifa ya Magharibi wanasema, wasi wasi kuu ya Bwana
Brahimi, wakati wa mazungumzo hayo siku ya Ijumaa, ni kuhakikisha kuwa
hakuna pande ambayo itaondoka na kususia mazungumzo hayo.
Hata hivyo wajumbe hao hawatarajiwi kushauriana moja kwa moja baada
ya kufanya kikao cha pamoja na bwana Brahimi, ripoti zinasema kuwa
watapewa vyumba tofauti ili kujadiliana wenyewe kabla ya kuwasilisha
mapendekezo yao.
Haijulikani mazungumzo hayo yataendelea hadi lini na wajumbe hao wanatarajiwa kupanga ratiba yake.
Serikali ya Syria inatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kupambana na
ugaidi huku upinzani ukiweka agenda kuu kuwa kuondolewa kwa rais Bashar
al-Assad.
Kiongozi wa Muungano wa Baraza la Kitaifa, Ahmed Jarba amewaambia
waandishi wa habari kuwa, jamii ya kimataifa kwa sasa imeridhika kuwa
rais Assad hatasalia madarakani kwa muda mrefu ujao.
0 comments:
Chapisha Maoni