Jumapili, Januari 05, 2014

MAN UTD YALIZWA NA SWANSEA


Timu ya soka ya Manchester United ya Uingereza imezidi kuandamwa na majanga baada ya kutupwa nje katika kombe la soka la mtoano baada ya kutandikwa mabao 2-1 na timu ya soka ya Swansea City. Manchester United imeadhirika na kuchezea kipigo hicho ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Old Trafford. Mambo yalionekana kuwa yasingekuwa mazuri katika mchezo wa jana tangu katika dakika za awali baada ya vijana wa Swansea kupachika bao la kuongoza katika dakika ya 13 kupitia mchezaji wake Wayne Routledge. Hata hivyo Javie Hernandez hakuwapa mashabiki wa Swansea City nafasi ya kushangilia sana kwani dakika tatu baadaye alisawazisha bao hilo. Timu mbili hizo zilikwenda mapumziko zikiwa zimefungana bao 1-1. Kipindi cha pili vijana wa Moyes walifanya kila jitihada kuhakikisha kwamba, hawaadhiriki lakini mambo yalionekana kuwa magumu. Dakika ya 81 Manchester United walipata pigo baada ya beki wake wa kulia Fabio kutolewa nje kwa kadi nyekundu zikiwa zimepita dakika sita tu tangu alipoangia uwanjani akichukua nafasi ya Ferdinand. Huku mashabiki wakidhani kwamba, mchezo huo utamalizika kwa matokeo ya mabao 1-1 na hivyo timu hizo kurejeana katika mechi nyingine kutafuta mshindi atakayesonga mbele, jahazi la Manchester United lilizama katika dakika ya 89 baada ya Bony kupachika bao safi na kuwaacha vinywa wazi mashabiki wa Man UN ambao hawakuamini walichokuwa wakikiona. Matokeo hayo yanazidi kumshinikiza mkufunzi wa timu hiyo David Moyes ambaye inaonekana mikoba ya Sir Alex Ferguson imemzidi uzito. Manchester United inashika nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu ya Primia nchini Uingereza ikiwa imejikusanyia pointi 34 tu katika mechi 20. Man U imetandikwa mechi sita katika ligi hiyo, imetoa droo mara 4 na kushinda mechi kumi tu.

0 comments:

Chapisha Maoni