Jumapili, Januari 05, 2014

MAABARA ZA SHULE CHANZO CHA UHALIFU WA TINDI KALI

Baada ya matukio ya watu kadhaa kumwagiwa tindikali nchini na kuacha sintofahamu katika jamii, imebainika kuwa shule ndizo zinazoongoza kwa kuwa na shehena nyingi ya tindikali ambayo imepatikana bila kupitia utaratibu unaotakiwa.

Mashambulizi ya kutumia tindikali ambayo yaliwalenga watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini, wafanyabiashara na raia wa kigeni, yameacha hofu miongoni mwa wananchi kutokana na kutapakaa kwa tindikali mitaani.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Meneja wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Mashariki, Daniel Ndiyo, alisema imebainika kuwa watumiaji  wa kemikali 748 hawajasajiliwa na ofisi hiyo.
Alisema watumiaji  399 katika hao ni shule za sekondari.
Ndiyo alisema watumiaji hao walibainika katika operesheni ya kukagua na kusajili watumiaji wa kemikali, iliyofanyika Septemba na Oktoba mwaka jana.
Kutajwa kwa watumiaji wasiosajiliwa kunaweka bayana namna ambavyo watu waliokuwa wakitekeleza mashambulizi ya kutumia tindikali walivyokuwa wakinunua ‘silaha’ hizo kwa urahisi, hasa katika maduka binafsi na shule za sekondari.
“Eneo kubwa ambalo tulikuwa hatujalikagua ni shule za sekondari. Shule hizi haziagizi kemikali kutoka nje ya nchi. Zinanunua kutoka kwa hawa wasambazaji wadogo, kwa hiyo kitu cha kwanza ambacho tulitaka kufanya ni kuchunguza ili tujue mtu anayeingiza kemikali nchini anamuuzia nani,” alisema Ndiyo.
Operesheni hiyo ilifanikisha kutambuliwa kwa wafanyabishara wakubwa 43 wa jijini Dar es Salaam, ambao huingiza kemikali na kuiuza kwa wateja nchi nzima.
Pia alisema kutokana na kutokuwepo kwa udhibiti imara wa ununuzi wa kemikali, kuna uwezekano kuwa hata wateja wadogo nao walikuwa wanauza kwa watu wengine mitaani.
Hata hivyo, Ndiyo hakuwa tayari kutaja aina ya tindikali ambayo inapatikana kwa wingi mitaani kwa madai kuwa kufanya hivyo kutachochea watu wasiokuwa  na nia njema kuitafuta tindikali hiyo kwa ajili ya kuwadhuru watu wengine.
Katika kudhibiti madhara makubwa zaidi kutokea, mtu yeyote haruhusiwi kununua kemikali bila ya kuwa na cheti au kibali kutoka kwa Mkemia Mkuu kinachomruhusu kununua bidhaa hiyo.
“Hata wafanyabiashara wadogo wa kutengeneza sabuni wanapaswa waje hapa (Ofisi ya Mkemia Mkuu) wajisalimishe na kujieleza wao ni kina nani na wanafanya nini, ili waandikiwe barua na kuwekwa kwenye rekodi kwamba wao wanatumia kufanyia kitu fulani,” alisema.

0 comments:

Chapisha Maoni