Jumatano, Januari 29, 2014

KIAMA CHA DIAMOND NA WEMA SEPETU KIMEFIKA, PANGA MAALUM KUTUMIKA!!!

HABARI mpya! Mama wa Miss Tanzania 2006/07, Wema Isaac Sepetu, Mariam Sepetu anadaiwa kuingia rasmi mitaani akiwasaka wapenzi, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Wema.

Kwa mujibu wa chanzo hicho makini, mama Wema ameamua kuchukua uamuzi huo baada ya kusikia taarifa kutoka kwa watu kwamba, Diamond amekuwa akisambaza maneno mitaani kuwa haogopi vitisho vya mwanamke huyo kufuatia hatua yake ya kumrudia binti yake.
Hivi karibuni, mama Wema alizungumza na wanahabari,  na kusema kitendo cha Diamond kumrudia bintiye hakubaliani nacho.
Aliongeza kuwa, kufuatia hatua hiyo iko siku ataingia mtaani kumsaka Diamond na popote pale atakapomnasa, atamkata na panga.
“Jamani si mnakumbuka juzikati mama Wema alisema atamsaka Diamond? Sasa amesikia Diamond anatangaza mitaani kwamba, hatishiki na tamko la mama mkwe wake huyo na watakapokutana watajua nani zaidi.
“Hivi ninavyosema, mama Wema ameingia mtaani kuwasaka. Lengo lake awakute wote wawili ili awaanzishie timbwili la kufa mtu.
“Tangu Ijumaa iliyopita, kila siku anatoka kwenda mitaani kuwasaka, naamini siku akiwakuta pamoja kweli itakuwa vita kubwa,” kilisema chanzo chetu.
 Chanzo kilipoulizwa kama kweli mama Wema amepania kuwanasa wawili hao, kwa nini asiwafuate nyumbani kwa binti yake, Kijitonyama, Dar ambako wanapika na kupakua, kilijibu:
“Ameweka mtego wake pale, bahati mbaya sana Diamond naye anaishi kwa machale. Kuna siku anakwenda kulala kuna siku haendi. Huenda na yeye (Diamond) ameweka watu wake ndani kwa Wema wa kumpelelezea kama mama Wema atakwenda au ana dalili za kwenda.”
Chanzo kikaendelea: “Siku hizi Diamond anaweza kwenda kwa Wema, akaacha gari lake na kutoka na la Wema na kurudi kwake usiku sana.”
Baada ya kuzinyaka nyeti hizo, Amani liliamua kuutafuta ukweli ambapo Jumanne iliyopita lilimsaka mama Wema kwa njia ya simu lakini iliita bila kupokelewa.


Baada ya dakika tano, mama huyo mwenye ‘machungu’ na mwanaume yeyote anayemchezea bintiye alituma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) akisema: Nipo msibani tuma sms. Pia akatuma sms kwenye simu ya pili akisema: Nipo msibani, ulikuwa unasemaje?
Mwanahabari alimtumia madai yote kuhusu yeye kuanza kuwatafuta Wema na Diamond, pia likamjulisha kwamba kama anawatafuta kweli, muda huo, wawili hao walikuwa wapo chumbani kwa Wema hawajaamka.
Hata hivyo, mama Wema hakujibu meseji yoyote kati ya hizo mbili hali iliyotafsiriwa na Amani kuwa, uchungu wa msiba ulimuondolea uwezo wa mawasiliano.
Mapaparazi wetu walitia timu nyumbani kwa Diamond, Sinza-Mori na kukutana na mtu mmoja aliyedai ni mjomba wa staa huyo ambaye alidai Diamond Platnumz alitoka asubuhi na mama yake, Sanura Kassim kwenda Tegeta, Dar.
NYUMBANI KWA WEMA
Baada ya kutoka nyumbani kwa Diamond huku wakiamini Mbongo Fleva huyo kaenda Tegeta kama alivyosema mjomba mtu, mapaparazi walikwenda nyumbani kwa Wema.
Baada ya kugonga geti kwa dakika moja, alitokea mlinzi na mambo yalikuwa kama ifuatavyo;
Paparazi: Mambo?
 Mlinzi: Poa, karibu.
Paparazi: Asante, nina shida na Wema, sijui nimemkuta?
Mlinzi: Wamelala, hawawezi kuamka muda huu.
Paparazi: Wamelala? Nani na nani?
Mlinzi: Madam (Wema) na Diamond.
 Paparazi: Ina maana Diamond yumo ndani?
Mlinzi: Si nimekwambia wamelala?
Paparazi wetu alifanikiwa kupenyeza macho kwenye nafasi ya uzio na kuyaona magari ya wote wawili, la Diamond aina ya Toyota Land Cruiser V8 na la Wema, Toyota Lexus Harrier.

SOURCE: GPL

0 comments:

Chapisha Maoni