Jumatatu, Januari 27, 2014

HABARI KUTOKA BBC ZINASEMA KUWA KIONGOZI WA AL SHABAAB AMEUAWA KWA KOMBORA

Wakaazi wa Kusini mwa Somalia, wameambia BBC kuwa kamanda mmoja mkuu wa kundi la wanamgambo la Al Shabaab ameuawa katika shambulizi la kombora.
Shambulizi hilo lilifanywa na wanajeshi wa Marekani.
Wamesema kuwa kamanda huyo Sahal Iskudhuq, na wapiganaji wengine wanne wa kundi hilo, wameuawa kwenye shambulizi hilo.
Kombora liligonga gari la wanamgambo hao ambalo walikuwa wanasafiria karibu na mji wa pwani wa Barawe.
Taarifa hizi hata hivyo bado hazijathibitishwa na jeshi la Marekani.
Iskudhuq inasemekana alikuwa na uhusiano wa karibu sana na kiongozi wa Al Shabaab Ahmed Abdi Godane na kamanda mkuu wa kitengo cha ujasusi cha kundi hilo kijulikanacho kama Amniyat.
Al Shabaab wameondoka kutoka katika miji mikubwa ya Somalia ikiwemo Mogadishu ingawa bado wanadhibiti sehemu kubwa za nchi.

0 comments:

Chapisha Maoni