Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili, Dk Marina Njelekela amesema saratani ya matiti inaongoza kwa
kuwa na waathirika wengi zaidi ukilinganisha na saratani nyingine.
Akifungua mafunzo ya kuwapiga msasa madaktari wa
upasuaji wa matiti, Dk Njelekela alieleza kuwa kwa kipindi cha mwaka
mmoja jumla ya wagonjwa 856 waliofanyiwa upasuaji katika vitengo viwili
vya upasuaji kati yao 162 waligundulika kuwa na saratani ya matiti.
“Yapo magonjwa mengi yanayoshambulia matiti
yakiwamo vivimbe na maambukizi, lakini saratani inaonekana kuzidi kuwa
tishio kwa wanawake ndiyo maana tumeamua kuendesha mafunzo haya ili
kuwapa ujuzi zaidi madaktari” alisema Dk Njelekela.
Alisema kutokana na hali hiyo, Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili imeamua kutoa mafunzo kwa madaktari wa hospitali kadhaa za
Jiji la Dar es salaam zikiwamo za Temeke, Amana, Mwanayamala, Regency na
IMTU ili kujifunza tiba na njia mpya za kukabiliana na tatizo hilo.
Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye
ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Ugiriki, Profesa
Zervoudis Stephane alikiri kuwepo ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani
ya matiti duniani na matibabu yake pia yamekuwa yakibadilika kila siku
kulingana na ukuaji wa teknolojia.
Kwa mujibu wa Profesa Stephane, upasuaji
unafanyika kwa teknolojia ya hali ya juu zaidi ambapo sindano huchomwa
katika eneo husika na kufuatiwa na upasuaji mdogo ili kuondoa sehemu
iliyoathirika.



0 comments:
Chapisha Maoni