Jumatano, Septemba 04, 2013

MWANAMKE AKAMATWA NA KONYAGI FEKI MBEYA

Mwanamke mmoja anashikiliwa na jeshi la polisi baada ya kukutwa akiuza pombe kali aina ya Konyagi bandia katika duka lake jana majira ya saa 06:45 mchana katika eneo la Mbalizi, Wilaya ya Mbeya vijijini mkoani Mbeya.
Taarifa toka kwa maafisa wa polisi zinasema kuwa mtuhumiwa huyo aliyefahamika kwa jina la Eliza Shija, 28, Msukuma, Mfanya biashara na mkazi wa Mbalizi amekamatwa na askari polisi wakiwa katika msako maalumu kwa kushirikiana na maafisa wa kampuni ya Konyagi kutoka makao makuu Dar es Salaam kwa kosa la kukutwa akiuza pombe bandia zilizo na jina la kampuni hiyo.
Habari zaidi zinasema kuwa mtuhumiwa amekutwa na katoni 117 za chupa ndogo za Konyagi na dazani 9 za konyagi maarufu kama Viroba ambazo zote ni bandia lakini thamani halisi ya bidhaa bado haijapatikana.
Taratibu za kumfikisha mahakamani mtuhumiwa zinaandaliwa huku mshtakiwa akiwa bado mahabusu.
Pamoja na hayo kaimu kamanda wa polisi mkoa wa mbeya, Kamishna msaidizi wa jeshi la polisi Barakael Masaki anatoa wito kwa wafanya biashara kuacha tabia ya kuwa na tamaaya kujipatia utajiri wa haraka kwa njia ya zisizo halali kwani ni kinyume cha sheria.
Aidha anatoa rai kwa kwa jamii hasa watumiaji wa vinywaji vya aina zote kuwa makini wakati wa ununuzi na utumiaji wa bidhaa hizo kwani nyingine si salama kwa matumizi ya binadamu na pindi wakiwabaini watoe taarifa katika mamlaka husika ili sheria zifuate mkondo wake.

0 comments:

Chapisha Maoni