Timu ya Simba imeshinda mechi yao dhidi ya timu ya SC Villa ya
Uganda kwa mabao 4-1 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliochezwa
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mashujaa wa Simba katika mchezo huo walikuwa ni
viungo, Jonas Mkude, Willium Lucian na Betram Mombeki akipachika mabao
mawili huku bao la kufutia machozi kwa SC Villa likifungwa na Ronald
Mganga.
SC Villa ilianza mchezo vizuri na kupata bao la
kwanza katika dakika ya tisa lililofungwa na Mganga akiunganisha kwa
shuti kali krosi ya Sijar Jamal iliyoshindwa kuokolewa na mabeki wa
Simba.
Baada ya bao hilo, Simba waliamka na kufanikiwa
kusawazisha goli hilo kupitia kiungo Mkude ambaye alifunga bao hilo kwa
shuti akiwa nje ya eneo la 18 baada ya kupokea pasi ya Amri Kiemba.
Kiungo Lucian aliyeingia kuchukua nafasi ya Humud
alipatia Simba bao la pili katika dakika ya 54 kwa shuti la umbali wa
mita 26 akimalizia pasi ya Kiemba.
Mshambuliaji Mombeki alipachika bao la tatu katika
dakika ya 70, akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Said Ndemla na
kugonga mwamba na kumkuta mfungaji.
Dakika tatu baadaye Mombeki alipachika bao la nne akiunganisha krosi ya Nassoro Masoud Cholo.
Nayo Coastal Union ililazimishwa suluhu na Three Pillars kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, leo watashuka dimbani kumenyana na Waganda hao kwenye Uwanja wa Taifa.
Yanga inajiandaa na mechi yao ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam ambayo inajifua Afrika Kusini.
Kingilio katika mchezo huo ni VIP Sh20,000, VIP B
Sh15,000, VIP C Sh10,000, wakati viti vya rangi ya machungwa, bluu na
kijani ni Sh5,000.
0 comments:
Chapisha Maoni