Mgombea urais wa muungano wa
upinzani nchini Kenya National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga
amepinga matokeo ambayo yanaendelea kutangazwa na tume ya uchaguzi
nchini humo, IEBC.
Bw Odinga amewaambia wanahabari kwamba tume hiyo imekuwa ikitangaza matokeo kwenye tovuti yake na kufuata utaratibu ufaao.
Waziri
mkuu huyo wa zamani amesema kabla ya matokeo yoyote kutangazwa, IEBC
inafaa kuwapa maajenti wa vyama Fomu 34A kutoka vituoni.
Amesema kwa sasa, bila kuwepo kwa fomu hizo, ni vigumu kubaini matokeo yanayopeperushwa yanatoka wapi.
"Mfumo
umeacha kufanya kazi. Sasa ni mitambo inayopiga kura. IEBC wamesema
kwamba hakuna chama chochote kilichopinga matokeo. Lakini vyama
vitapingaje matokeo bila kujua asili yake? Ni fomu 34A pekee
zinazoonesha chanzo cha matokeo," amesema.
"Kwa hivyo, tunakataa
matokeo yote yaliyotangazwa kwa sasa na kuitaka tume ya IEBC itoe fomu
34A za kila kituo kabla ya matokeo zaidi kutangazwa."
IEBC imekuwa
ikitangaza matokeo ya urais mtandaoni, na kufikia saa tisa na robo
alfajiri, matokeo hayo yalikuwa yanamuonyesha Rais Uhuru Kenyatta wa
chama cha Jubilee akiwa mbele na kura 6331140 (55.27%) naye Bw Odinga
akiwa na kura 5031737 (43.92%).
Matokeo hayo ni ya kutoka vituo 295319 kati ya vituo 40883 nchini humo.
"Hii ni kompyuta inayopiga kura," alisema Bw Odinga akikataa matokeo hayo.
Hali
ya wasiwasi imekuwa ikitanda katika kituo cha taifa cha kujumlishia na
kutangaza matokeo katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi.
Matokeo
yalianza kutiririka baadaye Jumanne jioni baada ya shughuli ya
kuhesabiwa kura kuanza. Matokeo hayo yamekuwa yakionesha Bw Kenyatta
akiongoza.
Wakala
mkuu wa muungano huo wa upinzani, naibu waziri mkuu wa zamani Musalia
Mudavadi alikuwa awali amehutubia wanahabari na kutaja matokeo
yanayotangazwa na tume hiyo kama utapeli.
Alitoa wito kwa wafuasi wa muungano huo kupuuzilia mbali matokeo yanayotangazwa.
0 comments:
Chapisha Maoni