Kwa mara nyingine tena mvutano wa kisiasa
umeigubika nchi ya Afrika Kusini kiasi kwamba, maelfu ya wapinzani wa
serikali wameendelea kufanya maandamano katika siku za hivi karibuni
wakitaka Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo ajiuzulu.
Maelfu ya wapinzani wamefanya
mkusanyiko mkubwa jirani na jengo la Mahakama ya Katiba
mjini Johannesburg na kutangaza kwamba, mudhahara na mkusanyiko huo wa
malalamiko utaendelea hadi pale Rais Zuma atakapojiuzulu na kuachia
madaraka ya nchi. Baleka Mbete, Spika wa Bunge la Afrika Kusini amesema
kuwa, wapinzani hao wamewasilisha barua ya mashtaka dhidi ya serikali
kuhusiana na kura ya siri ya kutokuwa na imani na serikali katika Bunge
la nchi hiyo. Mahakama hiyo inatarajiwa kutangaza msimamo wake kuhusiana
na upigaji kura wa siri kuhusiana na kutokuwa na imani na Rais Jacob
Zuma.
Licha ya kuwa kabla ya hapo pia Rais Zuma aliandamwa na wimbi la
upinzani kutokana na tuhuma za ufisadi wa fedha na wapinzani kumtaka
ajiuzulu, lakini duru mpya ya mivutano baina ya serikali yake na
wapinzani ilianza mwishoni mwa mwezi Machi, baada ya Rais huyo
kulifanyia marekebisho baraza lake na mawaziri na kumtupa nje ya baraza
hilo Pravin Gordhan aliyekuwa Waziri wa Fedha.
Akihalalisha uamuzi wake huo, Rais Zuma
alisema kuwa, mabadiliko hayo yalifanyika katika fremu ya juhudi za
kuboresha hali ya uchumi na kuondoa vizingiti vya sasa vya kiuchumi.
Hata hivyo watu wengi wanaamini kwamba, mabadiliko hayo yalitokana na
vita vya madaraka ndani ya chama tawala cha ANC na kwamba, kufutwa kazi
Pravin Gordhan kulifanyika kwa matashi ya kisiasa.
Pravin Gordhan alikuwa waziri kuanzia
mwaka 2009 hadi 2014 na baadaye mwishoni mwa mwaka jana akateuliwa tena
kushika wadhifa huo. Tangu alipoteuliwa tena kuchukua wadhifa wa Waziri
wa Fedha, Pravin Gordhan amekuwa na mivutano na shakhsia wa kisiasa wa
chama tawala cha ANC. Mivutano baina ya Pravin Gordhan na wanasiasa hao
ilianza baada ya waziri huyo aliyefutwa kazi kusisitiza juu ya ulazima
wa kupambana na uongozi mbaya na kuweko marekebisho katika muundo wa
mashirika ya kiserikali nchini. Aidha alisisitiza mara chungu nzima juu
ya ulazima wa kupambana na ufisadi.
Pravin Gordhan alikuwa na mpango wa kupunguza matumizi ya serikali,
aongeze kodi na kuifikisha nakisi ya bajeti ya nchi hadi asilimia 3.2 ya
uzalishaji malighafi katika mwaka wa fedha wa 2016-2017. Mbali na
kuibuka mivutano iliyotokana na kuuzuliwa waziri huyo, kuenea ufisadi,
kukosekana nafasi za ajira na kupungua kiwango cha ukuaji uchumi ni
sababu nyingine zinazotajwa na wajuzi wa mambo kwamba, zimepelekea
kuongezeka malalamiko katika nchi hiyo dhidi ya serikali.
Afrika Kusini ni moja ya nchi
zinazosafirisha nje ya nchi madini, lakini kwa miaka kadhaa ya hivi
karibuni kutokana na kupungua bei ya madini chimbuko lake likiwa ni
kupungua wateja hususan wanunuzi wakubwa kabisa kama China, imekuwa
ikikabiliwa na matatizo ya kifedha na kiuchumi.
Kuongezeka kiwango cha kupanda gharama
za maisha, kukata tamaa wawekezaji, mashirika na watumiaji kuhusu
mustakabali wa uchumi wa Afrika Kusini ni sababu nyingine ya kudorora
kiwango cha ukuaji uchumi wa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo,
katika miaka kadhaa ya huko nyuma, Afrika Kusini ilikuwa nchi yenye
mafanikio makubwa zaidi ya ukuaji wa uchumi.
Suala la kupambana na ufisadi lingali ni takwa la akthari ya
wapinzani wa Rais Jacob Zuma. Wapinzani wanamtuhumu Zuma kwamba,
hapambani na ufisadi na rushwa kama inavyotakiwa.
Hivi sasa sio wapinzani tu wanaotaka
Rais Zuma ajiuzulu, bali hata maveterani wa vita vya ubaguzi wa rangi
nchini humo, wanaharakati wa chama tawala, muungano wa wafanyakazi na
makundi ya kiraia nchini humo nayo yamejiunga katika safu ya wanaotaka
Zuma aachie ngazi kabla ya kumalizika muhula wake wa pili wa uongozi.
Akthari yao wana wasiwasi kwamba,
kupungua uungaji mkono wa wananchi kwa chama hicho kutakuwa na taathira
hasi kwa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa 2019. Pamoja na hayo
yote, Rais Zuma amesisitiza kuwa, atabakia madarakani hadi muhula wake
wa kisheria utakapomalizika.
0 comments:
Chapisha Maoni