Rais wa Tanzania John Magufuli amepangiwa kufanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi hiyo tangu kuingia madarakani mwaka jana.
Dkt Magufuli anatarajiwa kuzuru nchi jirani ya Rwanda Jumatano na Alhamisi, kufuatia mwaliko kutoka kwa Rais Paul Kagame.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wizara ya mambo ya nje ya Tanzania, Dkt Magufuli na Bw Kagame watafungua daraja la kimataifa la Rusumo na kituo cha huduma za pamoja mpakani katika mpaka wa Tanzania na Rwanda.
Baadaye, wataelekea Kigali ambapo watafanya mazungumzo ya pamoja.
Dkt Magufuli pia ataweka shada la maua katika makumbusho ya mauaji ya kimbari ya Rwanda 1994 mjini humo.
“Ikizingatiwa kwamba hii ndiyo ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu achukue madaraka Oktoba 2015, ziara hii inaashiria umuhimu ambao Tanzania inaweka katika kuimarisha uhusiano wake na majirani zake.”
Rais Magufuli amekuwa mapumzikoni nyumbani kwake eneo la Chato, kaskazini magharibi mwa Tanzania.
0 comments:
Chapisha Maoni