Jumanne, Januari 19, 2016

KUHUSU UPOTOSHWAJI WA GAZETI LA MWANAHALISI KUHUSIANA NA UCHAGUZI WA UBUNGE JIMBO LA KIJITOUPELE

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inapenda kutaarifu Umma na Watanzania kwa ujumla kuwa Jimbo la Kijitoupele lililoko Zanzibar ni miongoni mwa Majimbo hamsini(50) ambayo yalitegemewa kufanya uchaguzi mkuu tarehe 25, oktoba,2015.
Hata hivyo Jimbo hilo halikufanya uchaguzi wake wa Mbunge kutokana na hitilafu katika karatasi za kupigia kura badala Wapiga kura walishiriki katika kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Tume imefikia uamuzi wa kutoa ufafanuzi huu kutokana na taarifa iliyochapishwa na gazeti la MwanaHalisi toleo l Na.322 la Januari 18, 2016 katika ukurasa wake wa mbele likidai “ NEC YAIBUA MAPYA” Habari hii si sahihi na inalenga kuupotosha umma na kuleta uchochezi miongoni mwa Wananchi.
Kwa ujumla maelezo yote yaliyopo katika taarifa hiyo yanaeleza kwamba, Tume imeanzisha Jimbio jipya, kwa mujibu wa taarifa ya gazeti husika ni Jimbo la Kijitoupele – Zanzibar.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda inasisitiza kuwa taarifa zilizotolewa na Gazeti la MwanaHALISI siyo za kweli, ni za uongo, uzushi, uzandiki na uchochezi. Kufuatia taarifa hiyo,Tume inapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:
• Tarehe 13 Julai, 2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari ikionesha Orodha ya Majimbo yatakayofanya uchaguzi wa Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na Jimbo la Kijitoupele lipo katika Orodha hiyo. Taarifa hii ipo katika tovuti ya Tume.
• Katika Taarifa hiyo, Tume ilieleza wazi kuwa Majimbo ya Zanzibar yataendelea kuwa hamsini (50), ingawaje Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeongeza majimbo manne na kuwa Hamsini na Nne (54).
• Tulieza sababu ya kubaki na Majimbo hamsini (50) ni kutokana na matakwa ya Ibara ya 98 (1) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo ili kuongeza idadi ya wabunge kutoka Zanzibar inahitaji theluthi mbili ya Wabunge kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge kutoka Zanzibar kuunga mkono mabadiliko hayo.
• Tulieza kuwa, kipindi hicho Tume isingeweza kuandaa na kuwasilisha Muswada Bungeni kwa kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilikuwa linamaliza muda.
• Katika taarifa hiyo, ilifafanuliwa kuwa, ili kubaki na majimbo Hamsini (50), kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, majimbo manne yaliunganishwa kwa ajili ya Uchaguzi wa Wabuge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaotoka Zanzibar.
• Majimbo yaliyounganishwa ni:
1. Jimbo la Bububu liliunganishwa na Jimbo la Mtoni, likaitwa jimbo la Bububu
2. Jimbo la Mwera liliunganishwa na Mto pepo likaitwa jimbo la Mwera
3. Jimbo la Kiembesamaki liliunganishwa na Chukwani likaitwa jimbo la Kiembesamaki
4. Jimbo la Pangawe liliunganishwa Kijitoupele likaitwa Kijitoupele
• Kwa mantiki hiyo Jimbo la Kijitoupele ni mojawapo ya Majimbo hayo (50) ambayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilisimamia na kuratibu Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wabunge.
• Tarehe 28 Oktoba, 2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa taarifa kwa Umma kuwa, ilishapokea Matokeo ya Kura za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa kutoka Majimbo yote ya Zanzibar na siyo “siyo Matokeo ya Ubunge”
• Tarehe 19 Desemba, 2015 Tume ilitoa orodha ya Majimbo ambayo hayajafanya Uchaguzi wa Wabunge tarehe 25 Oktoba, 2015 kutokana na hililafu mbalimbali, mojawapo ya majimbo hayo nane (8), jimbo la Kijitoupele - Zanzibar ni miongoni.
Ni vema wananchi wakafahamu kwamba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi haianzishi na haijaanzisha Jimbo jipya la Uchaguzi baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
Hii inaonesha ni kiasi gani Mhariri wa Gazeti la MwanaHALISI alivyodhamiria kuupotosha Umma kwani katika Makala/Taarifa hiyo hiyo ambayo anadai hakuna Jimbo la Kijitoupele (Unguja); anaeleza kuwa tarehe 25 Oktoba 2015 wapiga Kura wa Jimbo la Kijitoupele walikosa fursa ya kumchagua Mbunge. Amemtaja Mhariri wa Gazeti la MwanaHALISI kuwa ni Wapiga Kura wa Jimbo la Kijitoupele, ambalo anadai eti Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeliibua miezi mitatu baada ya Uchaguzi. Huu ni uongo na upotoshwaji wa makusudi kabisa.
Tume inapenda wananchi waelewe kuwa, hata kabla Tume ya Uchaguzi haijafuta matokeo wa Zanzibar, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilikuwa imesha tangaza kuahirisha Uchaguzi katika Majimbo nane (8) likiwemo la Kijitoupele kwa sababu za Vifo vya Wagombea na hitilafu mbalimbali.
Jimbo la Kijitoupele la Zanzibar ni miongoni mwa majimbo nane (8) ambayo yaliahirishwa kufanya uchaguzi wa Wabunge tarehe 25 Oktoba, 2015, ambapo majimbo sita (6) ambayo ni Lushoto, Ulanga Mashariki, Masasi Mjini, Ludewa, Handeni Mjini na Arusha Mjini yaliahirishwa kutokana na vifo vya wagombea na majimbo mawili (2) ya Kijitoupele - Zanzibar na Jimbo la Lulindi – Masasi yaliahirishwa kutokana na hitilafu mbalimbali.
Hoja nyingine iliyotolewa na gazeti hilo ilihusu uteuzi wa Uteuzi wa Wabunge wa Viti Maalum. Ifahamike kwamba katika maamuzi yake kuhusiana na viti maalum, Tume imezingatia matakwa ya Ibara ya 78 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayoeleza kuwa, ili chama kilichoshiriki Uchaguzi Mkuu kipate Viti Maalum ni lazima kiwe kimepata angalau asilimia tano (5%) ya Kura zote halali za Ubunge. Hivyo, Viti Maalum vilivyobaki haviwezi kugawanywa hadi hapo Jimbo la Kijitoupele litakapofanya Uchaguzi katika tarehe ambayo itaitangazwa na Tume hapo baadaye.
Mhariri wa Gazeti la MwanaHALISI alipaswa kufanya uchunguzi na uchambuzi wa kina kuhusu habari aliyoiachapisha ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na Viongozi wa Tume ya Uchaguzi ili wapate ufafanuzi wa Majimbo ya Uchaguzi na siyo kutoa Taarifa za uongo, uchochezi na upotoshaji kama walivyofanya.
Mhariri wa Gazeti la MwanaHALISI atambue uandishi wa habari ni zaidi ya kushika kalamu na kuandika, unahusisha uwezo wa kutafuta habari pande zote mbili ili kupata mizania ya habari anayoiandika, kufanya utafiti, kujiridhisha pasipo shaka kuwa habari anayoitoa ni sahihi.
Kwa kuwa Mhariri wa Gazeti la MwanaHALISI alikusudia kuupotosha umma kwa sababu anazozifahamu yeye mwenyewe kwa kutoa Taarifa zisizo sahihi, za uongo na uchochezi Tume ya Taifa ya Uchaguzi inamtaka Mhariri wa MwanaHALISI KUIOMBA RADHI TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI, UKURASA WA MBELE WA TOLEO LIJALO KAMA ALIVYOFANYA KATIKA GAZETI HILO.
Kama wasipofanya hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi italichukulia Gazeti la MwanaHALISI hatua za Kisheria.

0 comments:

Chapisha Maoni