Miaka 62 iliyopita muwafaka na leo, Jomo Kenyatta mwanaharakati, mwanasiasa na mpigania uhuru mashuhuri barani Afrika na Rais wa Kwanza wa Kenya alitiwa mbaroni kufuatia amri ya utawala wa kikoloni nchini Kenya. Mzee Kenyatta alikuwa miongoni mwa watu 100 mashuhuri nchini humo waliotiwa mbaroni katika kipindi cha masaa 24 ikiwa ni katika fremu ya mpango wa kuibana Mau Mau, kundi la wapiganaji wa Kenya waliokuwa wakiupinga utawala wa kikoloni wa Waingereza. Siku hii inajulikana nchini humo kuwa Siku ya Mashujaa.
Miaka 216 iliyopita kama leo, wananchi Waislamu wa Cairo waliendesha mapambano ya ukombozi dhidi ya maghasibu wa Kifaransa. Mapambano ya wananchi dhidi ya jeshi la Ufaransa yalianza huko Cairo baada ya Napoleon kuikalia kwa mabavu Misri. Siku hiyo wananchi wa Cairo sambamba na wanazuoni wa dini waliandamana na kukusanyika katika Chuo Kikuu cha Al Azhar. Vita vilianza kati ya wakazi wa Cairo wasio na silaha na askari jeshi wa Ufaransa waliokuwa wamejizatiti kwa silaha kufuatia amri iliyotolewa na Jenerali De Boer, kamanda wa kijeshi wa Ufaransa aliyetaka kukandamizwa wananchi. Baadaye wananchi wa Misri waliwaua wanajeshi wengi wa Ufaransa, akiwemo Jenerali De Boer.
Na miaka 187 iliyopita kama leo vita vya majini vya Navarino au The Battle of Navarino vilitokea katika ghuba ndogo ya Navarino kwenye bahari ya Mediterranean. Katika vita hivyo, meli za kivita za Uingereza, Russia na Ufaransa zilizishambulia meli za kivita za utawala wa Othmania kwa lengo la kuihami Ugiriki. Vita hivyo vilifikia tamati kwa kushindwa vibaya utawala wa Othmania.
0 comments:
Chapisha Maoni