Jumatatu, Julai 14, 2014

UKAWA WAMJIBU KIKWETE

Wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kupitia kwa Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, wamemjibu Rais Kikwete wakisema watakuwa radhi kurudi Bunge la Katiba endapo kutafanyika taathmini na tafakuri ya kina katika kubaini sababu za kuvurugika kwa Bunge hilo na kuzitazama kanuni zinazolisimamia, pamoja na sheria ya mabadiliko ya katiba.

Pia UKAWA wametaka pawepo na makubaliano ya maandishi kwamba hakutakuwa na kauli za matusi, kudharauliana wala kejeli, bali kitakachojadiliwa ni maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasmu ya Tume ya Jaji Warioba.
Msimamo huo ulitolewa juzi na Mhe.Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, alipokuwa akizungumzia mchakato huo wa Katiba mpya Wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, baada ya UKAWA kuwa wameombwa na Viongozi mbalimbali warudi Bungeni.
Alisema kuwa Viongozi mbalimbali akiwemo Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wamewaomba warudi kwenye Bunge hilo, lakini wai wametoa masharti kwamba kufanyike vikao vya pamoja vya kutathmini hali iliyojitokeza awali, kisha wawekeane utaratibu wa kufuata kimaandishi.
Uwendawazimu ni kufanya mambo yale yale kwa kutumia watu wale wale na kwa utaratibu ule ule, halafu utegemee matokeo tofauti. Tumetoka kwenye Bunge la Katiba ambapo tumeona matusi, kejeli, dharau, ubaguzi wa hali ya juu na kupuuzwa kwa maoni ya wananchi, halafu mnatuita turudi kwenye Bunge lile lile tukatukanane kisha mtegemee kupata Katiba bora
Alihoji Mbowe.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, alisisitiza kuwa, hata wakikubaliana wakarudi kisha matendo yale ya awali yakajitokeza ikiwemo kupuuza maoni ya wananchi, hawatasita kutoka tena kwa lengo la kupigania kupatikana kwa Katiba bora yenye kuzingatia maslahi ya wananchi wote.
Mhe.Mbowe alisema kuwa, Wabunge wa CCM hawawezi kuhitimisha mchakato huu wakiwa peke yao, kwa kile alichoeleza kuwa, Katiba inatakiwa kuandaliwa na makundi yote ya jamii.

0 comments:

Chapisha Maoni